Uhuru azungumza kuhusu BBI Amerika
Na CHARLES WASONGA
RAIS Uhuru Kenyatta alisifu mpango wa maridhiano (BBI) katika hotuba yake Jumatano, Februari 5, 2020, nchini Amerika anakohudhuria Hafla ya Kitaifa ya Maombi.
Akihutubia wanachama wa Baraza la Kujadili Masuala ya Uongozi maarufu kama Atlantic Council, Rais Kenyatta alisema mpango huo ni muhimu kwa uthabiti wa kitaifa baada yake kuridhiana kisiasa na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.
“Tumeanza kutekeleza mabadiliko ya kisiasa, kijamii na kiuongozi nchini Kenya kupitia mpango wa Maridhiano, BBI, ambao kimsingi ndiyo suluhu ya kinyumbani ya siasa za migawanyiko ambayo imezonga taifa letu kwa zaidi ya miaka 30,” Rais Kenyatta akawaambia wanachama wa baraza hili jijini Washington, kabla ya kuanza kwa Hafla ya Maombi ya Kitaifa.
Rais alisema BBI iliyotokana na handisheki kati yake na Bw Odinga inalenga kuondoa vita vya kila baada ya uchaguzi.
“Pili, inalenga kupalilia siasa ya ushirikishaji ambayo ni muhimu katika kunawiri kwa demokrasia katika taifa letu kwa kuachana na siasa za migawanyiko,” Rais Kenyatta akasema.
Akaongeza: “Tatu mpango huu utatusaidia kuweka misingi ya ukuaji wa kiuchumi na kupambana na zimwi la ukabila na janga la ufisadi.”
Rais Kenyatta alisema mataifa mengi barani Afrika na Asia yamefikia Kenya yakitaka kujifunza, kuiga na kutekeleza mpango kama huu wa BBI kama suluhu kwa changamoto zinazoyakabili.