HabariSiasa

Uhuru hakuchaguliwa kwa kuwa ametoka Mlima Kenya, Ruto amkosoa Waiguru

September 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

JOSEPH WANGUI na NDUNG’U GACHANE

NAIBU RAIS William Ruto amekosoa kauli ya Gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru kuhusiana na jamii inayofaa kuwania urais, akisema Rais Uhuru Kenyatta hakuchaguliwa kwa misingi ya kikabila.

Gavana huyo ameendelea kulaumiwa kwa kauli yake kwamba Wakenya hawako tayari kumchagua rais mwingine kutoka kwa jamii ya Agikuyu.

Bi Waiguru alisema kuwa kuna hatari ya jamii nyingine nchini kuhisi kutengwa, ikiwa rais atatoka katika jamii hiyo.

Akitetea mfumo wa serikali unaobuni nafasi za waziri mkuu na manaibu wake wawili, Bi Waiguru alisema kuwa ni jamii za Wakalenjin na Wakikuyu pekee ambazo zimekuwa zikishikilia urais.

“Ikiwa tutakuwa na nyadhifa nyingi serikalini, Wakenya watahisi wamewakilishwa vizuri na hakutakuwa na ghasia baada ya uchaguzi. Sitaki mfumo wa serikali ambapo anayeshinda urais anapata mamlaka yote,” akasema.

Hata hivyo, Naibu Rais alimwambia kuwa Rais Kenyatta hakuchaguliwa kutokana na jamii yake, lakini kwa uwezo wake wa kuongoza.

“Tulimuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta kumrithi Rais Mstaafu (Kibaki) kutokana na uwezo wake, lakini si kwa msingi wa kabila lake,” akasema Dkt Ruto, kwenye mtandao wa Twitter.

Akaendelea: “Rais Kenyatta si kiongozi wa kabila lolote, lakini wa Chama cha Jubilee (JP) ambacho ndicho chenye idadi kubwa zaidi ya madiwani, wabunge na magavana katika kaunti 41 kati ya 47 kote nchini. Tafadhali acheni kasumba ya ukabila.”

Kumekuwa na dhana kwamba Jopo la Maridhiano (BBI) lililobuniwa na Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga litatoa mapendekezo ya mageuzi ya katiba yanayowiana na kauli ya Bi Waiguru.

Malumbano hayo yakishika kasi, naye mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria ameionya mirengo ya kisiasa ya ‘Tanga Tanga’ na ‘Kieleweke’ kukoma kulumbana, akisema kuwa huenda Dkt Ruto na Bw Odinga wakaungana kisiasa.

Mirengo hiyo imekuwa ikimuunga mkono na kumpinga Naibu Rais William Ruto mtawalia katika ukanda wa Mlima Kenya.

Bw Kuria alisema ikiwa viongozi hao watachukua hatua hiyo, basi huenda jamii ya Agikuyu ikakosa kujumuishwa serikalini, hali ambayo itaiathiri sana kisiasa.

“Eneo la Mlima Kenya ndilo tishio kuu kwa ari za Bw Odinga na Dkt Ruto kushinda urais. Ikiwa wataungana, basi watashinda urais, hali ambayo italinyima nafasi ya kuwa serikalini kutokana na malumbano ya kisiasa yanayoendelea,” akasema.

“Nimekuwa katika mstari wa mbele kuwashinikiza viongozi wetu kuungana,” akasema Bw Kuria, kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo.’

Mnamo Jumapili, mbunge wa Makueni Daniel Maanzo aliwaonya baadhi ya wanasiasa kuwa mistakabali yao imo hatarini, ikiwa viongozi hao wawili wataungana.

“Wanasiasa wapya wanapaswa kutahadhari sana, kwani si vigumu kuwaona Bw Odinga na Dkt Ruto wakiungana na kufanya kazi pamoja, hasa baada ya kamati ya BBI kuwasilisha ripoti yake,” akasema Bw Maanzo.