Uhuru kimya hali ya nchi ikizorota
BENSON MATHEKA Na SAMMY LUTTA
KIMYA cha Rais Uhuru Kenyatta wakati serikali yake na nchi kwa jumla inakabiliwa na changamoto nyingi, kimechochea kila aina ya uvumi miongoni mwa wananchi kuhusu yanayoendelea serikalini.
Hii ni baada ya Rais Kenyatta kuendelea kunyamaza wakati ikiwa wazi chama chake cha Jubilee kimegawanyika, Baraza la Mawaziri haliko pamoja tena, uhusiano kati yake na Naibu Rais William Ruto umeharibika, wadogo wake serikalini wanampuuza, shughuli za kaunti zinakaribia kukwama na bei ya unga inazidi kupanda miongoni mwa masuala mengine.
Wadadisi wa siasa wanasema sauti ya kiongozi wa taifa inahitajika katika masuala haya na mengine yanayokumba taifa ili kukomesha uvumi ambao umeongezeka miongoni mwa wananchi kuhusu yanayoendelea serikalini.
Wanaeleza kuwa Wakenya wanamtazama yeye kama rais wao na wala sio mawaziri ama maafisa wengine, na makosa ya mawaziri ni makosa yake kwa sababu ni yeye aliyewateua.
Kwa muda sasa imekuwa wazi Jubilee kimegawanyika katika mirengo: ‘Tangatanga’ inayounga mkono Naibu Rais William Ruto, ‘Kieleweke’ kinachopigia debe handisheki ya Rais na Raila Odinga na ‘Team Wanjiku’ wanaodai kutetea mwananchi wa kawaida.
Licha ya tofauti hizi kuwa wazi, Rais Kenyatta hajachukua hatua za kurekebisha mambo na amekataa miiti ya kuitisha kikao cha kujadili hatima ya Jubilee akisema hana wakati wa kupiga siasa.
Tatizo lingine ambalo kiongozi wa taifa amenyamazia ni ukaidi wa wazi wa Dkt Ruto na mrengo wake wa ‘Tangatanga’ wa kuwataka wakomeshe siasa za uchaguzi mkuu wa 2022.
Sio mara moja ambapo Rais Kenyatta amewakemea ‘Tangatanga’ kwa kampeni hizo, lakini amekosa kufuatilia maneno yake kwa vitendo.
Wadadisi wa siasa wanasema japo kila Mkenya ana haki ya kutoa maoni, Rais anahitajika kutuliza hali hii ya kupuuzwa na wadogo wake kwa kuhakikisha nidhamu inadumishwa na kila mmoja serikalini.
Rais Kenyatta pia anakabiliwa na tatizo la migawanyiko katika Baraza la Mawaziri, ambapo duru za kuaminika zinasema kuna makundi matatu: Lake Rais Kenyatta, la Dkt Ruto na wachache wasioegemea upande wowote.
Hali hii ilizorota ilipodaiwa kuwa mawaziri wanne, Peter Munya, Joe Mucheru, Sicily Kariuki na James Macharia walikuwa na njama ya kumuua Naibu Rais.
Rais pia amenyamazia mvutano kuhusu uagizaji wa mahindi kutoka nje, ambalo ni suala muhimu kwa mwananchi wa kawaida kwani linahusisha unga ambao ni chakula kinachotegemewa na wengi.
Rais Kenyatta pia amekuwa kimya kuhusu mvutano kati ya magavana na serikali kuu kuhusu mgao kwa kaunti.
Hapo jana Gavana wa Kaunti ya Turkana, Josphat Nanok almtaka Rais alisema alichangia kuzuka kwa mzozo huo: “Rais Uhuru alitia sahihi sheria ya kuruhusu Serikali Kuu kutumia pesa katika bajeti ya 2019 bila kufuata utaratibu unaofaa,” akasema Bw Nanok.
Suala lingine ambalo Rais Kenyatta amekosa kuweka wazi ni mjadala wa wakereketwa wake ambao wanapendekeza atafutiwe wadhifa mkuu serikalini kupitia mageuzi ya kikatiba, wakisema angali na nguvu za kuendelea kuhudumu.
Japo hizi zinaweza kuwa siasa duni ambazo hafai kujihusisha nazo, wachanganuzi wanahisi kuwa ni suala la umuhimu kwa taifa na sauti yake inahitajika ili kuweka msimamo wake wazi.