Uhuru na Ruto waongezewa mshahara
Na BERNARDINE MUTANU
RAIS Uhuru Kenyatta na naibu wake Dkt William Ruto watapata nyongeza ya mshahara ya asilimia 3.9.
Nyongeza hiyo iliondolewa hapo 2017 wakati wa uchaguzi, pamoja na nyongeza ya viongozi wengine wakuu serikalini kukabiliana na ongezeko la mzigo wa mishahara nchini.
Kulingana na stakabadhi rasmi kutoka kwa Hazina Kuu, mshahara wao utaongezwa kutoka Sh36.6 milioni kwa mwaka hadi Sh38 milioni.
Baada ya kukatwa kwa nyongeza hiyo, mshahara wa rais ulipungua kutoka Sh1.65 milioni hadi Sh1.44 milioni na naibu wake kutoka Sh1.4 milioni hadi Sh1.23 milioni.
Nyongeza hiyo imepangiwa kutekelezwa wakati Hazina ya Fedha inalenga kuongeza kiwango cha fedha za maendeleo na huduma za kimsingi kama vile usalama, afya na elimu.
Lakini kumekuwa na changamoto ya uokotaji wa mapato, hali ambayo ililazimisha Hazina ya Fedha kutathmini bajeti yake.
Viongozi hao wawili pia watapata marupurupu ya Sh15.2 milioni kwa mwaka, mwaka wa kifedha unaoanzia Julai 2019.
Mshahara kwa wote wawili utakuwa ni Sh22.8 milioni kwa mwaka, hivyo kiwango cha jumla kitakuwa ni Sh38 milioni.
Hata hivyo, mshahara na marupurupu hayo, utakuwa wa chini ikilinganishwa na kabla ya Juni 2017, ambapo walikuwa wakipata kiwango cha jumla cha Sh51.2 milioni, kabla ya kiwango hicho kupunguzwa.
Mishahara ya viongozi hao wawili wakuu pamoja na maafisa wengine wa serikali ilikatwa kabla ya uchaguzi
Nyongeza kwa wakuu hao wa nchi inajiri wakati hazina kuu inaweka mikakati ya kupunguza pesa zinazoelekezwa katika miradi ya maendeleo hasa sekta muhimu kama Usalama, Afya na Elimu.
Serikali imekuwa ikipambana na uhaba mkubwa wa fedha kutokana na kutofikisha viwango vinavyolenga vya ushuru unaokusanywa, tatizo ambalo lililazimisha hazina kuu kuangalia bajeti yake upya mara kwa mara.