Ukweli kuhusu 'Punguza Mzigo'
Na BENSON MATHEKA
WAKENYA wana nafasi ya kujinasua kutoka kwa minyororo ya utumwa wa Wabunge ambao wamekuwa wakijiongezea pesa wanavyotaka na serikali ya kitaifa inayojivuta kutoa pesa kwa serikali za kaunti kwa kupitisha mswada wa Punguza Mzigo kwenye kura ya maamuzi.
Mswada huo ambao umeungwa na wapigakura zaidi ya 1.2 milioni unapendekeza kuwa, idadi ya wabunge ipunguzwe kutoka 417 hadi 147, kutetea usawa wa jinsia na kupunguza wabunge wa kuteuliwa.
Pendekezo hili likipitishwa, chama cha Thirdway Alliance kilichoandaa mswada huo kinasema kwamba, Wakenya watakuwa wamepunguza gharama ya kuendesha bunge kutoka Sh36.8 bilioni hadi Sh5 bilioni kwa mwaka.
Hii inamaanisha kwamba, Wakenya wataokoa Sh31.8 bilioni kwa mwaka ambazo zinaweza kutumiwa kwa maendeleo.
Aidha, chama hicho kinachoongozwa na Wakili Ekuro Aukot kinapendekeza kuwa, mishahara ya rais na wabunge iwekwe kwenye katiba hivi kwamba, hawataweza kujiongezea marupurupu wanavyotaka.
Kulingana na mswada huo, mshahara wa Rais unapaswa kuwa Sh500,000 na wa wabunge Sh300,000 kwa mwezi.
Vita vya ubabe
Kwa kupitisha mswada wa marekebisho ya Katiba wa Punguza Mzigo, Wakenya watamaliza vita vya ubabe kati ya maseneta na wabunge kwa kufanya seneti kuwa na mamlaka zaidi.
Iwapo utapitishwa, mzozo unaoshuhudiwa kwa sasa kati ya seneti na Bunge la Kitaifa kuhusu mgao wa mapato utakuwa jambo la sahau kwa sababu kaunti zitakuwa zikitengewa asilimia 35 ya mapato ya serikali badala ya 15 ilivyo kwa sasa.
Seneti itakuwa na uamuzi wa mwisho kuhusu mgao wa mapato kwa serikali za kaunti.
Ili kutia nguvu ugatuzi, mswada huo unapendekeza wadi zote 1450 nchini ziwe kitovu cha maendeleo ili kuhakikisha wapigakura wanafaidika zaidi.
Hii itamaanisha kuwa wapigakura watafuatilia kwa karibu miradi wanayotaka katika eneo lao na kufuatilia utekelezaji wake kwa karibu.
Kama sehemu ya kufanikisha hili, chama hicho kinasema hazina ya maeneobunge ifutiliwe mbali na pesa hizo kupatiwa serikali za kaunti.
Wadhifa mwingine ambao utafutwa kupunguza gharama ikiwa mswada huo utapitishwa kwenye kura ya maamuzi ni wa naibu wa magavana.
Kipindi kimoja
Bw Aukot anapendekeza kuwa Rais awe akihudumu kwa kipindi kimoja cha miaka saba na kustaafu ili kuondoa ushindani wakati wa uchaguzi marais wanapotetea viti vyao.
Hatua hii, anaeleza, itaepusha nchi na ghasia zinazoshuhudiwa wakati wa uchaguzi.
Anatoa mfano wa ghasia zilizotokea nchini mwaka 1992 Daniel Moi alipokuwa akitetea kiti cha urais, 2007/2008 Mwai Kibaki alipokuwa akigombea kwa kipindi cha pili na cha mwisho na 2017 Rais Kenyatta alipokuwa akitetea kiti chake.
Kenya haikukumbwa na ghasia baada ya uchaguzi wa 2002 na 2013 marais waliokuwa wakihudumu walipostaafu.
Ukipitishwa ulivyopendekezwa, haitawezekana kupanua muundo wa serikali ya kitaifa kwa kubuni wadhifa wa waziri mkuu na naibu wake, hatua ambayo itapunguza gharama ya kuendesha serikali.
Bw Aukot anasema marekebisho ambayo chama chake kimependekeza kwenye mswada huo yatasaidia kuokoa zaidi ya Sh3.78 trilioni kwa mwaka.
“Hizi ni pesa nyingi kuliko bajeti ya taifa na tutaweza kuajiri na kulipa walimu, wauguzi, madaktari wa kutosha na pia kubuni nafasi za kazi kwa vijana wetu ambao idadi yao inazidi kuongezeka,” Bw Aukot alisema kwenye taarifa alipokuwa akikusanya sahihi kuunga mapendekezo hayo.