Habari

Umeme warudishwa visiwani Pate na Faza baada ya majuma mawili ya 'kukaa gizani'

July 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na KALUME KAZUNGU

WAKAZI zaidi ya 3,000 wa visiwa vya Pate na Faza, Kaunti ya Lamu wamepata afueni baada ya kampuni ya kusambaza umeme nchini – Kenya Power – kuurejesha baada ya majuma mawili ya kukaa gizani.

Akithibitisha kurejeshwa kwa nguvu hizo za umeme, Meneja wa Mauzo wa Kenya Power, tawi la Lamu, Bernard Kataka, alisema hali hiyo ilitokana na hitilafu za mitambo ya jenereta zilizokuwa zikitumika eneo hilo.

Bw Kataka alisema ofisi yake ilifanya jitihada na kuleta mitambo mipya ili kuhudumia wateja eneo hilo.

Alisema mitambo iliyoletwa imesaidia kutatua kikamilifu hitilafu iliyokuwa ikishuhudiwa eneo hilo mara kwa mara na kuwataka wakazi kuondoa hofu.

“Haya majuma mawili yamekuwa ni kipindi kigumu kwa wakazi wa Faza na Pate, lakini tunawashukuru wateja wetu kwa kutuvumilia hadi tukasuluhisha tatizo,” akasema Bw Kataka.

Mapema juma hili, wakazi wa kisiwa cha Faza walishiriki maandamano na kufululiza hadi kwenye ofisi za Kenya Power eneo la Faza kushinikiza kurudishwa kwa stima eneo hilo.

Wakazi hao wakiongozwa na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake, Bi Ruweida Obbo waliikashifu kampuni hiyo kwa utepetevu katika kushughulikia hitilafu za umeme kila mara zinapotokea eneo la Lamu Mashariki.

Sehemu mojawapo ya kisiwa cha Faza. Picha/ Kalume Kazungu

“Mimi binafsi nimekuwa nikisukuma bungeni ili visiwa hivi vya Pate na Faza viunganishwe kwa stima. Tulitarajia stima ingekuwa imerudishwa kufikia Juni 27. Hatutaondoka kituoni hapa Faza. Tutalala hapa hadi pale mtakapoturudishia stima,” akasema Bi Obbo.

Baadhi ya wafanyabiashara waliozungumza na Taifa Leo pia waliishinikiza kampuni hiyo kuwafidia hasara walizokadiria kwa majuma mawili bila stima eneo hilo.

“Vitu vyetu vilivyokuwa kwenye majokofu viliharibika kutokana na kukosekana kwa stima kipindi kirefu hivyo ni vyema tufidiwe,” akasema Bw Abdalla Ali.