Habari

Ushahidi dhidi ya mganga wa Kangundo wakosekana, aachiliwa huru

October 18th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

NA RICHARD MUNGUTI

MGANGA maarufu wa Kangundo, Kaunti ya Machakos, Bi Annah Mutheu Ndunda (pichani) aliyekamatwa wiki iliyopita kwa tuhuma za kushiriki katika wizi wa magari na visa vya uhalifu aliachiliwa Alhamisi na Mahakama ya Nairobi baada ya polisi kukosa ushahidi wa kumfungulia mashtaka.

Hakimu mkazi Bi  Electer Rianyi alimwachilia Bi Mutheu baada ya afisa aliyekuwa anachunguza kesi hiyo kusema “sikupata ushahidi wa kutosha kuweza kumfungulia mashtaka mshukiwa.”

Mutheu alitiwa nguvuni mnamo Oktoba 9, 2018 pamoja na Bw John Macharia Kiragu.

Maafisa wa Polisi wa kitengo cha kupambana na uhalifu almaarufu Flying Squad (FS) walimtia nguvuni Mutheu na kumsafirisha kutoka Tala, kaunti ndogo ya Kangundo.

Alisafirishwa hadi makao makuu ya FS kumchunguza ikiwa alikuwa anashiriki katika uhalifu baada ya polisi kupata magari matano likiwemo lori.

Bali na magari hayo muundo wa Toyota na Isuzu, Mutheu alikutwa na Vitambulisho vya kitaifa 112.

Afisa aliyekuwa anachunguza kesi hiyo Konstebo James Mwangi alimfikisha Mutheu na Bw Kiragu mbele ya Bi Rianyi na kuomba aamuru wazuiliwe kwa muda wa siku 10 ndipo akamilishe uchunguzi.

“Naomba hii mahakama iamuru washukiwa hawa wazuiliwe katika kituo cha polisi kuhojiwa na kuwasaidia Polisi kuchunguza iwapo magari yaliyokutwa katika makazi ya Mutheu yameibwa ama yameripotiwa kupotea,” alisema Konstebo Bw Mwangi Oktoba 9 2018.

Pia alieleza korti kuwa anataka kuwasiliana na idara ya usajili wa magari na mamlaka ya uchukuzi NTSA kubaini wenye magari hayo.

Afisa huyo pia alimweleza hakimu kuwa atachunguza vitambulisho hivyo kuwatambua wenyewe katika idara ya usajili wa watu.

Pia polisi walikuwa wanachunguza vitambulisho hivyo kubaini ikiwa ni halali. Mutheu na Kiragu walipinga wakizuiliwa kwa muda wa siku 10 na kuomba waachiliwe kwa dhamana.

Bi Rianyi aliwaachilia kwa dhamana ya Sh150,000. Polisi wamekamilisha uchunguzi lakini hawakupata ushahidi wa kutosha kuwawezesha kumfungulia mashtaka Mutheu na Kiragu.

Mutheu alijipatia umaarufu kwa kuwafanya watu waliotekeleza uhalifu kukamatwa na walalamishi ama kurudisha mali waliyodaiwa wameiba.