Habari

Utata zaidi ripoti ikiashiria Walibora aliuawa

April 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

POLISI sasa wameshinikizwa kutoa video za kamera za CCTV zitakazosaidia kutegua kitendawili cha kifo cha Prof Ken Walibora.

Wakenya mitandaoni jana walisema, video hizo zitatoa majibu ya wakati na jinsi msomi huyo aliyeegesha gari lake katika Barabara ya Kijabe, alivyofika Muthurwa inakodaiwa aligongwa na matatu ya kampuni ya Double M.

Inadaiwa Prof Walibora alikuwa akiwatoroka watu, ambao huenda ndio waliomkata mkononi kwa kisu.

Kupitia Wanjiku Revolution, Wakenya jana waliungana kutaka Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH) ieleze kwa nini Prof Walibora hakutibiwa kutoka saa nne asubuhi hadi alipokata roho saa sita za usiku.

Afisa wa Mawasiliano wa KNH, Bw Hezekiel Gikambi ambaye pia ni rafiki wa marehemu, alisema hospitali hiyo itatoa kauli rasmi hii leo.

Ripoti ya mwanapatholojia mkuu wa serikali, Johansen Oduor, inaonyesha kuwa, kifo cha Prof Walibora kinazingirwa na utata.

“Tuliona majeraha kwenye upande wa kulia wa kichwa, mkono wa kulia ulikuwa umevunjika na damu ilikuwa imevuja ubongoni. Isitoshe, kulikuwa na jeraha fulani kwenye mkono wa kulia ambao ulionyesha kwamba alikuwa amedungwa kwa kisu chenye makali au jora. Jeraha hilo linaloibua shaka, lilikuwa katikati ya kidole gumba na cha shahada,” akasema Oduor.

Kulingana na ripoti ya awali ya polisi, Prof Walibora alionekana akikimbia kutoka vichochoro vya eneo la Muthurwa mwendo wa saa tatu asubuhi mnamo Ijumaa ya Aprili 10, 2020 akivuka Barabara ya Landhies.

“Alikuwa akifukuzwa na kundi la watu walioonekana kuwa vijana wa mtaa; yaani ‘chokoraa’. Alifaulu kuvuka upande mmoja wa barabara ya kuingia jijini. Alipofikia upande wa pili wa barabara ya kutoka jijini, alijigonga kwa gari la kwanza kabla ya basi la Double M lililokuwa likiendeshwa kwa kasi kumpiga dafrau,” akasema mmoja wa walioshuhudia kisa hicho.

Madai mengine ambayo yametolewa ni kwamba, Prof Walibora alikuwa ameelekea katika eneo la Muthurwa kusemezana na dereva wa lori aliyekuwa amsafirishie vifaa vya ujenzi nyumbani kwake katika Kaunti ya Trans-Nzoia.

OCPD wa Kituo cha Polisi cha Central, Bw Mark Wanjala, jana alisisitiza kuwa uchunguzi kuhusiana na kifo cha Prof Walibora sasa umetwaliwa na maafisa wa DCI.