UVUNDO: Wakazi Tononoka wataka sehemu mbadala itafutwe kwa ajili ya soko
Na MISHI GONGO
WAKAZI wanaoishi katika eneo la Tononoka mjini Mombasa, wameiomba serikali ya kaunti hiyo itafute sehemu mbadala kuweka soko.
Wanasema kuwa tangu kufunguliwa kwa soko eneo hilo, wamekuwa wakivumilia uvundo unaosababishwa na bidhaa zilizooza na uchafu.
Machi 20, 2020, serikali ya kaunti ilitangaza kufungwa kwa soko la Kongowea kwa muda kama njia mojawapo ya kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona na hapo ikageuza uwanja wa Tononoka kuwa soko wazi.
Baadhi ya wauzaji waliokuwa katika soko la Kongowea walielekezwa kuuza bidhaa zao katika uwanja huo.
Hata hivyo, wakazi sasa wanalalamikia harufu mbovu inayotokana na uchafu wa mboga zilizooza na wameitaka kaunti kepeleka wauzaji maeneo mengine mbali na makazi ya watu.
Mkazi wa eneo hilo Bw Said Ali, akiongea na ‘Taifa Leo’ mnamo JumapiliĀ aliitaka kaunti ibuni mikakati itakayohakikisha kuwa wauzaji wanadumisha usafi au kuwatafutia sehemu mbadala.
“Tunalazimika kuvumilia uvundo kutoka kwa makabeji na viazi vilivyooza; uvundo huo unatukosesha amani, tunataka kaunti kuhakikisha kuwa usafi unadumishwa,” akasema.
Alisema anahofia mkurupuko wa maradhi iwapo hali hiyo haitadhibitiwa.
“Uvundo kutoka kwa uchafu huo unaleta nzi na tunahofia kupata ugonjwa wa macho na kipindupindu,” akaeleza mkazi huyo.
Mkazi mwingine Bi Mariam Mohammed alisema harufu hiyo mbovu inaingia majumbani mwao hivyo kuwakosesha hewa safi.
“Kaunti inapaswa kuwalazimisha wauzaji hawa kusafisha maeneo wanakouzia kila jioni, kwa sababu mabaki ya mboga na matunda huoza na kuozeana na kuleta harufu mbaya,” akasema.
Bi Mohammed alisema japo kaunti ilichukuwa uamuzi huo kukabili corona, wakuu wasiposisitiza usafi basi kuna uwezekano wa kuzuka maradhi mengine kama kipindupindu.
Aidha alisema kuwa japo serikali iliwaleta wauzaji katika eneo hilo ili kuwawezesha kuwa na umbali wa mita moja baina yao na hata wateja ili kukinga maambukizi ya corona, wauzaji hao bado hawajatekeleza sheria hiyo.
“Hatuelewi ni kwa nini wameletwa sehemu hii kwa sababu bado tunashuhudia msongamano miongoni mwao na wateja,” akasema.