Habari

Vibanda haramu kunakofyonzwa mafuta Industrial Area vyaangushwa chini

Na SAMMY KIMATU May 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ZAIDI ya vibanda 150 vinavyoshukiwa kutumiwa katika kufyonza mafuta mkabala wa barabara ya Nanyuki-Nairobi katika eneo la Viwandani vilibomolewa Alhamisi na serikali kwa kunyima serikali ushuru mkubwa kwa biashara hiyo ya magendo.

Wakati wa msako huo ulioongozwa na naibu kamishna wa kaunti ndogo ya Makadara, Bw Philip Koima zoezi hilo lilikabiliwa na maandamano kutoka kwa raia.

Walakini, uwepo mkubwa wa maafisa wa polisi wa kupambana na ghasia na wenzao waliovalia kiraia walidhibiti hali hiyo.

Tingatinga labomoa vibanda haramu, majiko na maeneo ya kufyonza mafuta katika barabara ya Nanyuki Eneo la Viwanda Picha|Sammy Kimatu

Bw Koima alisema kushirikishwa kwa umma na uhamasishaji kupitia mikutano ya hadhara kulifanyika mara kwa mara kukiongozwa na kikosi cha usalama cha kaunti ndogo na viongozi wa serikali ya kaunti.

“Tulikuwa na ushiriki wa umma mara kadhaa uliohudhuriwa na washikadau husika, tukatoa notisi kwa wamiliki wa vibanda kuondoka eneo lililolindwa na lililotangazwa kwenye Gazeti la Serikali lakini walikaidi,” Bw Koima alisema.

Alieleza mpango wa operesheni hiyo uliohusisha kubomolewa kwa vibanda vyote haramu na kuwakamata watakaobainika kujihusisha na biashara haramu ndani ya eneo la Bohari za Mafuta.

Wamiliki wa kampuni zinazofanya kazi ndani ya Barabara ya Nanyuki walishauriwa kufanya usanifu wa ardhi kando ya kuta zao ili kuzuia wanyakuzi wa ardhi na kulinda mali yao.

Wakati wa mashauriano, ilikubaliwa kwamba mashirika yote yataimarisha ufuatiliaji ili kukomesha mara moja shughuli yoyote haramu au unyakuzi wa ardhi na kuonywa kwamba watakaopatikana wamevamia ardhi hiyo wote watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, hakuna mtu aliyekamatwa baada ya washukiwa “kudokezwa juu ya operesheni hiyo mapema,” kulingana na mdokezi wetu.

Mnamo 2011, mkasa wa moto ulitokea mtaa wa mabanda wa Mukuru-Sinai ambapo moto kutoka bomba la mafuta ulisababisha mlipuko mkubwa na moto, na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 100 na uharibifu mkubwa.

Hali ilivyo baada ya ubomozi wa vibanda haramu, majiko na maeneo ya kufyonza mafuta katika barabara ya Nanyuki Eneo la Viwanda. Picha|Sammy Kimatu

Moto huo ulitokana na kuvuja kwa bomba la kampuni ya Kenya Pipeline Company (KPC), hali iliyopelekea mafuta kumwagika kwenye bomba la maji taka na kuwaka. Mkasa huo uliangazia hatari inayokodolea macho wakazi wa mabanda wanaokaa karibu na maeneo ya viwandani na ukosefu wa tahadhari.

Mamia ya nyumba na biashara ziliharibiwa, na maelfu ya watu walilazimika kuyahama makazi yao.

Mkasa huo ulizua ghadhabu na hasira, huku wengi wakilaumu KPC na serikali kwa uzembe na ukosefu wa hatua za usalama.

Tukio hilo liliibua wasiwasi kuhusu usalama wa miundombinu ya viwanda katika maeneo yenye watu wengi.

Vilevile, tukio hilo lilisababisha uchunguzi na kesi za kisheria dhidi ya KPC, ikiangazia hitaji la itifaki bora za usalama na ushirikiano wa jamii, kama ilivyoripotiwa na Business & Human Rights Resource Centre.