Vijana wachoma picha
VALENTINE OBARA na MARY WAMBUI
MASAIBU yanayomkumba Seneta wa Nairobi, Bw Johnson Sakaja ambaye alikamatwa kwa kukiuka kanuni za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona, yameibua upya mjadala kuhusu uwezo wa vijana kusimamia masuala ya nchi vyema kuliko wenzao wenye umri mkubwa.
Bw Sakaja, ambaye jana alitangaza kujiuzulu kutoka kwa uenyekiti wa kamati ya muda ya Seneti inayosimamia masuala ya Covid-19, alikuwa amenaswa na polisi katika baa saa za kafyu Jumamosi usiku.
Alipojisalimisha jana katika kituo cha polisi cha Kilimani, seneta huyo ambaye amekuwa akijizolea sifa kwa kuonekana kuwa kiongozi muungwana, aliweka dhamana ya Sh10,000 pesa taslimu akitarajiwa kufikishwa mahakamani leo.
“Nitafuata sheria, hakuna mtu ambaye ana mamlaka yanayozidi sheria. Sheria itatumiwa kwangu sawa na inavyotendeka kwa Mkenya mwingine yeyote,” akasema, akiandamana na wakili wake, Bw John Khaminwa.
Kisa hiki kimeongeza orodha ya viongozi vijana ambao wanakabiliwa na sakata mbalimbali ambazo zinatilia doa imani kuwa ni wakati wa vijana kuleta uongozi bora nchini.
Wakati huu, Gavana wa Nairobi Mike Sonko, 45, angali anakumbwa na kashfa ya ufisadi ambayo imemfanya kuzuiwa kuingia afisini mwake.
Bw Sonko, ambaye amewahi kukiri kuwa mfungwa zamani, hulaumiwa kwa mienendo yake ambayo huonekana kukiuka maadili ya uongozi ikiwemo kuonekana mlevi na kutumia matusi hadharani.
Katika kaunti hiyo hiyo, Mbunge wa Embakasi Mashariki, Bw Babu Owino, 30, anakumbwa na kesi kuhusu jaribio la mauaji.
Sawa na Bw Sonko, mbunge huyo alipata umaarufu kupitia kwa mienendo yake ya kuvuka mipaka ya maadili anapojitafutia umaarufu wa kisiasa.
Wakati mmoja, alijipata mashakani alipomtusi Rais Kenyatta wakati wa kampeni za uchaguzi.
Katika eneobunge jirani la Embakasi ya Kati, Mbunge Benjamin Gathiru pia alinaswa na polisi mapema Aprili alipopatikana katika baa Ruai.
Mbunge huyo mynyamavu alikamatwa pamoja na watu wengine waliokuwa naye kwani hilo lilikuwa ni ukiukaji wa kanuni za kuepusha maambukizi ya virusi vya corona.
Ingawa baadhi ya wananchi walimtetea Bw Sakaja na kusema hafai kuingizwa kwenye orodha ya watovu wa uadilifu kwa vile ‘kuteleza sio kuanguka’, wengine walisisitiza ameonyesha sura yake kamili.
“Seneta Sakaja ameomba msamaha kwa umma akakiri alikosea. Sote hukosea. Inahitaji ukuu kwa yeyote yule kukiri na kukubali kuadhibiwa kwa makosa yake. Yaishe,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Kuanisha Filamu Kenya (KFCB), Dkt Ezekiel Mutua.
Lakini mchanganuzi wa masuala ya uongozi, Bw Gabriel Oguda, alisema Wakenya wanapotoka wanapotetea viongozi kwa msingi kwamba hawakujua walichokuwa wanafanya wakiwa walevi.
“Johnson Sakaja ni sawa na Mike Sonko, isipokuwa tu kwamba hakutoroka kutoka gerezani. Wale wanaosema hakujua alichokuwa anafanya, ni wale wale ambao humwita Babu Owino muuaji kwa (kudaiwa) kufyatua risasi akiwa mlevi na bila kujua alichokuwa akifanya. Kwa mara nyingine, Wakenya wanakosa msimamo,” akasema.
Mbunge wa Starehe, Bw Charles Njagua almaarufu Jaguar pia amewahi kukamatwa mara kadhaa kwa madai ya uchochezi. Kando na hayo, alikumbwa pia na kesi za kusababisha ajali barabarani katika hali ya kutatanisha.
Tabia hizi za viongozi vijana hazionekani Nairobi pekee.
Katika Kaunti ya Nandi, Gavana Stephen Sang, 36, alikamatwa na kushtakiwa alipoongoza wakazi kuharibu shamba la kibinafsi la majani chai.
Na katika Kaunti ya Kilifi, Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, 45, alikamatwa alipohusishwa na ufyatuaji risasi ambapo mfuasi wa Chama cha ODM, Ngumbao Jola aliuawa.
Kisa hicho kilitokea usiku wa kuamkia uchaguzi mdogo wa Wadi ya Ganda, nyumbani kwa mgombeaji wa ODM, Bw Reuben Mwambire.
Katika Kaunti ya Murang’a, Mbunge wa Kiharu, Bw Ndindi Nyoro alikamatwa mwaka uliopita kwa kuhusishwa na rabsha zilizotokea kanisani.
Mbunge huyo alikuwa amelalamika kwamba, Mbunge Maalumu Maina Kamanda aliandaa harambee katika kanisa hilo lililo eneobunge lake bila kumwarifu.
Miongoni mwa mawaziri, aliyekuwa Waziri wa Michezo, Bw Rashid Echesa, alitimuliwa kwa sababu zisizojulikana na sasa anakumbwa na sakata ya kandarasi bandia ya silaha ya Sh39 bilioni.
Katika mwaka wa 2018, Rais Uhuru Kenyatta hakuficha hisia zake kuhusu vijana ambao wameshindwa kuafiki kiwango cha matarajio katika uongozi wao, akatetea anavyopenda kuajiri wazee kushikilia nyadhifa muhimu serikalini.