HabariHabari za Kaunti

Viongozi Lamu wataka ujenzi wa barabara msituni Boni ukamilishwe kutokomeza ugaidi

Na KALUME KAZUNGU August 11th, 2024 2 min read

WABUNGE na madiwani wa Kaunti ya Lamu wanaishinikiza serikali ya kitaifa kuweka kipaumbele ujenzi wa barabara zinazofahamika kuwa za kiusalama eneo hilo.

Mbunge wa Lamu Mashariki, Bi Ruweida Obbo, madiwani Omar Bwana (Kiunga) na Barissa Deko (Basuba), wamelalamikia kujikokota kwa ujenzi na upanuzi wa barabara unaoendelea.

Barabara hizo ambazo karibu zote hupitia ndani ya msitu wa Boni ni pamoja na Hindi-Bar’goni-Boni-Kiunga, Lamu-Ijara-Garissa na ile ya Mkokoni-Madina-Kiunga.

Viongozi hao wanalalamikia jinsi wananchi wanavyosumbuka kila kukicha kwa kukosa huduma muhimu, ikiwemo zile za hospitali, vitambulisho na kadhalika, kutokana na kwamba maeneo wanayoishi yanakosa barabara za kusafiria.

Bi Obbo alisema baadhi ya wananchi wameishia kuugua msongo wa mawazo kutokana na hali ngumu wanazokabiliana nazo maeneo yao.

“Ningeomba serikali iharakishe ujenzi wa barabara za kiusalama msituni Boni na mpakani mwa Kenya na Somalia. Wananchi wanalia kila siku kwa kukosa usafiri kwani barabara zote ziko vibaya,” akasema Bi Obbo.

Aliwafokea wanakandarasi waliopewa zabuni ya kuzijenga na kuzipanua barabara za kiusalama msitu wa Boni na Lamu Mashariki kwa jumla, akiwataka kukabidhi zabuni hizo kwa wanakandarasi wenyeji wa Lamu ili ujenzi uharakishwe.

“Najua serikali ilitenga karibu Sh1 bilioni kutekelezea ujenzi wa barabara zetu za kiusalama msituni Boni. Ikiwa mwenye zabuni hiyo anahofia usalama, basi aipeane kwa mwanakandarasi wa papa hapa nyumbani ili aharakishe ujenzi. Watu wangu wanateseka,” akasema Bi Obbo.

Naye diwani wa Kiunga, Omar Bwana, alisema kuboreshwa kwa uchukuzi eneo hilo pia kutafaulisha vita dhidi ya Al-Shabaab.

Bw Bwana alisema haipendezi kuona kwamba raia na walinda usalama wanahangaika kila wanapotaka kusafiri kutokana na barabara mbaya.

“Ninaamini endapo barabara zitaboreshwa eneo hili basi itakuwa rahisi kwa walinda usalama wetu kusafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine, hivyo kufaulisha operesheni inayoendelea dhidi ya magaidi. Wananchi wetu pia itakuwa rahisi kwao kuzifikia hospitali kama vile King Fahd,” akasema Bw Bwana.

Kwa upande wake, Diwani wa Basuba, Barissa Deko alisema mbali na kuboresha barabara, pia kuna haja ya serikali kuzifungua zahanati zote zilizofungwa msituni Boni.

Mnamo 2014, zahanati za Milimani, Basuba na Mararani zilifungwa kufuatia mashambulio yaliyokithiri kutoka kwa Al-Shabaab.

Ni zahanati mbili pekee za Kiangwe na Mangai ambazo kwa sasa zinahudumia wakazi wa msitu wa Boni japo vituo hivyo vya afya bado vinakabiliwa na ukosefu wa dawa na wahudumu wa afya.

“Mbali na kuziboresha barabara zetu, pia wahakikishe kila kijiji cha msitu wa Boni kinajengewa zahanati kuhudumia watu wake,” akasema Bw Deko.