Visiwa vya Mombasa na Manda huenda vikazama – Wanasayansi
Na WINNIE ATIENO
WANASAYANSI wameonya huenda visiwa vya Mombasa na Manda vikazama kufuatia mabadiliko ya tabianchi.
Kulingana na wanasayansi hao visiwa hivyo eneo la Pwani ya Kenya huenda vikazama kwa kipindi cha miaka 30 au 50 ijayo endapo juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuongezeka kwa kina cha maji baharini hazitazingatiwa.
Wanasayansi hao kutoka kwa Taasisi ya Utafiti wa Maswala ya Bahari na Samaki nchini Kenya yaani KMFRI wanaonya kuwa samaki katika bahari hiyo wako katika hatari ya kupotea huku mabaki ya plastiki yakisheheni Bahari Hindi.
Hii ni kwa sababu ya mienendo mibovu na mazoea ya baadhi ya Wakenya kutupa baharini bidhaa za plastiki ambazo zinaendelea kuchafua mazingira hayo.
Hata hivyo, wanasayansi hao wamebaini kuwa Wakenya wana fursa ya kubadilisha mkondo huo endapo watachukulia swala la uhifadhi wa mazingira kwa umakini na kulipa kipaumbele.
“Tunaweza kuokoa hali hii ili visiwa vyetu kuepuka majanga ya mabadiliko ya tabianchi. Sehemu hatari ni uwanja wa ndege pale Manda; sehemu inayotazamiwa kuzama kwenye Bahari Hindi mwaka 2030 au 2050 sababu iko mita moja kutoka kwa kingo za bahari. Kisiwa cha Mombasa pia kiko hatarini,” alisema Afisa Mkuu Mtendaji wa KMFRI Prof James Njiru.
Kwenye mahojiano na Taifa Leo mnamo Jumatano, mwanasayansi huyo aliwahakikishia Wakenya kwamba kuna juhudi za serikali, wanaharakati na mashirika ya uhifadhi wa mazingira kuokoa visiwa hivyo maarufu katika utalii.
“Bahari ni muhimu sana kwani tunapata manufaa mengi ikiwemo chakula (samaki), dawa, utalii, uchukuzi miongoni mwa mengine mengi. Lakini bahari zetu ziko katika hatari. Na tunapoadhimisha siku ya Bahari Ulimwengini hatuna budi kuwaelimishe Wakenya kuhusu hatari tunayokodolea macho ili tupate mshawasha wa kuhifadhi mazingira yetu,” alisema Prof Njiru wakati wa mahojiano.
Alisema kadri wakenya wanapotupa plastiki baharini nazo samaki zinasalia kuwa hatari ya kula uchafu huo.
“Mwaka 2050 plastiki zitakuwa nyingi kuliko samaki baharini. Tutakuwa na tani milioni 50 za plastiki kuliko samaki. Utakuwa unakula plastiki nyingi kuliko samaki. Lakini kama tutakoma kutupa plastiki basi tutaokoa samaki na mazingira baharini,” akasema Prof Njiru.
Katibu Mkuu katika Wizara ya Maswala ya Bahari na Samaki Prof Micheni Ntiba anawasihi Wakenya kupanda miti ili kuhifadhi mazingira.
Kwenye kikao na wanasayansi, Prof Ntiba alisema mvua inaponyesha na kusababisha maafa hususan katika sehemu za Pwani na Nyanza sababu kuu huwa ni athari hasi za uharibifu wa mazingira.
“Tukipanda miti kila mahali halafu mvua kubwa inyeshe, maji hayo yatamezwa ardhini badala ya kuteremka na kusababisha mafuriko baharini na sehemu za ziwa kama vile huko Nyanza kama inavyoendelea kushuhudiwa kwa sasa. Washikadau wote washirikiane na serikali kupanda miti ili kuepuka mmomonyoko wa ardhi,” Prof Ntiba akasisitiza.
Alisema Wakenya waliadhimisha siku ya Bahari Ulimwenguni wakati wa janga la corona ambalo limesababisha kusitishwa kwa kongamano muhimu wa Umoja wa Mataifa ambapo wenyeji washirika au wenza yalikuwa ni mataifa ya Kenya na Ureno.
Kongamano hilo la 2020 UN Ocean Conference lilikuwa lifanyike Juni 2 hadi 6 Kenya ikiwa mwenyeji wake.
Dkt James Kairo alisema mmomonyoko wa ardhi sehemu ya Pwani husababishwa kwa njia mbili.
“Ama kupitia wanadamu au ile njia ya kawaida (naturally mediated). Ile ya wanadamu hufanyika wakati miti ya bahari ambayo inazuia uchafuzi wa mazingira hayo na uharibifu huo hususan mikoko, nyasi za baharini (seagrasses) na miamba ya matumbawe yaani coral reefs huharibiwa. Inafaa tulinde mazingira yetu,” alisisitiza.