Habari

Ghasia zaendelea bunge la Nairobi kuhusu Elachi

October 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na COLLINS OMULO

VUTA n’kuvute kwa mara nyingine imeshuhudiwa tena katika Bunge la Kaunti ya Nairobi Nairobi madiwani wakikabiliana kuhusu hoja mpya ya kutaka kumtimua Spika Beatrice Elachi.

Wawakilishi wa wadi kutoka Bunge la Kaunti ya Nairobi wamekabiliana Jumanne kuhusu njama ya baadhi yao ya kutaka kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani na Spika Beatrice Elachi.

Vurugu hizo zilianza wakati mrengo unaomuunga mkono Bi Elachi, ulipovamia mkutano uliokuwa ukihutubiwa na wenzao ambao wanarindima ngoma ya Kiongozi wa wengi Abdi Guyo, ambaye haonani uso kwa macho na spika huyo.

Ngumi na mateke yalitanda kote kila diwani kutoka kila mrengo akimsakama mwenzake huku wengine waliokuwa wakilemewa na vita hivyo wakiamua kukikimbilia usalama wao.

Mkutano wa madiwani wa mrengo wa Bw Guyo uliandaliwa kujibu ule uliokuwa umefanyika hapo awali wa wawakilishi wadi wanaompigia debe Bi Elachi kuendelea kushikilia wadhifa huo wa uspika.

“Mheshimu Bi Elachi na hatutaruhusu kikao chochote cha kuwahutubia wanahabari kiendelee hapa iwapo hamtamheshimu. Tumewavumilia ya kutosha,” wakasema madiwani wanaoegemea upande wa seneta huyo wa zamani.

Hata hivyo, mrengo wa Bw Guyo umedai kwamba una amri kutoka mahakamani inayomzuia Bi Elachi kuongoza mjadala wowote bungeni hadi kesi waliyowasilisha isikizwe na iamuliwe.

Walidai kwamba tayari wamemkabidhi Karani wa bunge hilo Jacob Ngwele nakala ya hoja ya kumtimua spika huyo afisini ambayo ilitiwa saini ili kuzithibitisha kisha kuziwasilisha mbele ya madiwani kwa upigaji kura.

“Tutawasilisha hoja hiyo wakati wa kikao cha mchana ambacho kitaongozwa na naibu spika au diwani mwengine ambaye anatoka kwenye jopo la maspika washikilizi. Tunamtaka Bi Elachi aheshimu amri hii ya korti jinsi ambavyo tuliheshimu ile ilimrejesha afisini,” akasema Bi Chege Waithera diwani wa South B ambaye pia ni kiranja wa wengi kwenye bunge hilo.

Awali mrengo wa Bi Elachi uliahidi kumg’oa Bw Guyo kwenye wadhifa wake wa kiongozi wa wengi huku wakiahidi kwamba spika huyo habanduki kamwe.

“Sisi tupo nyuma ya spika na kumwondoa ni jambo lisilowezekana. Kujaribu kumbandua ni kama kuchapa mijeledi farasi mfu,” akasema diwani wa Dandora Charles Thuo.

Diwani huyo amefichua kwamba mpango wote wa kumwondoa Bw Guyo afisini tayari umekamilika sababu kuu ikiwa ni uongozi wake wa kiimla na kiburi kingi.

“Bw Guyo lazima ajiuzulu kama bado ana wakati. Tunaendea kumg’oa kwa kuwa yeye si kiongozi wa wengi tena. Hawezi kuwa anapigana na kila mtu na shughuli katika kaunti hazitokama kuendelea kwa sababu ya vituko vyake,” akasema Bw Thuo.