Waasi watamuweza Uhuru?
WABUNGE wa Jubilee wanaoegemea mrengo wa Naibu Rais William Ruto sasa wanapanga kuwasilisha hoja bungeni ya kuwatimua afisini mawaziri wanaodai wanaendesha njama ya kumhujumu Dkt Ruto.
Katika hatua inayolenga Rais Kenyatta ambaye kikatiba ndiye huwateua mawaziri, wabunge hao wanataka kuchunguza kile wanachodai kuwa sakata ya utoaji zabuni kwa polisi kwa lengo la kupendekeza adhabu kali kwa maafisa katika afisi ya Rais.
Wakiongozwa na Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungwa na mwenzake wa Kiharu Ndindi Nyoro, wabunge hao sasa wanaonekana kumkabili Rais Uhuru Kenyatta moja kwa moja katika mipango hii.
Hivi ndivyo vitisho vya moja kwa moja kwa serikali ya Rais Kenyatta kutoka kwa wabunge kutoka Mlima Kenya, ng’ome ya Rais Kenyatta.
Wanafanya hivyo kwa kutisha kumng’oa afisini Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i na kumhusisha Katibu katika wizara hiyo, Dkt Karanja Kibicho na sakata ya utoaji zabuni ya bima ya polisi.
Rais Kenyatta amewatwika, Dkt Matiang’i na Dkt Kibicho jukumu la kusimamia wizara ya usalama wa ndani wa nchi na ushirikishi wa shughuli za serikali yake.
“Ikiwa mtu anadhani tutaishi kwa woga na kulazimishwa kufuata mkondo fulani wa kisiasa, enzi hizo zimepita,” Bw Ichung’wa alisema.
Ameelekeza ghadhabu zake kwa Dkt Kibicho akisema ndiye amekuwa akimhujumu Dkt Ruto mbali na kuwaagiza polisi kususia mkutano wake juzi katika kaunti ya Nyeri.
“Kibicho ni nani kwa Naibu Rais aliyechuguliwa na mamilioni ya Wakenya kuitisha ratiba ya ziara zake,” Bw Ichung’wa akauliza.
Naye Bw Nyoro anadai maafisa fulani katika afisi ya Rais walipeana zabuni ya utoaji huduma za bima kwa polisi kwa kampuni iliyodai Sh1.7 bilioni na kuacha ile iliyotaja bei ya Sh628 milioni, hatua ambayo ni kinyume cha sheria.
“Sasa tutauliza maswali kuhusu bima ya polisi katika afisini ya Rais. Tutataka kujua ni kwa nini kampuni iliyoitisha pesa nyingi ndio ilipewa zabuni hiyo badala ya ile iliyotaja bei ya chini,” alisema Nyoro ambaye ni mwanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu (PAC).
Wabunge hao wanaonekana kukasirishwa na kuondolewa kwa walinzi wa baadhi ya majuzi, hatua waliofasiri kama adhabu kwao kuunga mkono azma ya Dkt Ruto kuingia Ikulu 2022.
Walinzi
Kando na Ichung’wa, wengine waliopokonywa walinzi na wameonakana kukaidi wito wa Rais Kenyatta kusitisha kampeni za mapema ni; Kimani Ngunjiri (Bahati), Mary Njoroge (Maragua), Susan Kihika (Seneta, Nakuru) na Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu.
Wengine ni Sabina Chege (Mwakilishi wa Wanawake Murang’a), Alice Wahome (Kandara), Rigathi Gachagua (Mathira) na Catherine Waruguru (Laikipia).
Hata hivyo, itakuwa kibarua kigumu kwa wabunge hao kufanikisha azma yao ya kumng’oa Dkt Matiang’i kutoka wadhifa wake kupitia hoja bungeni kwa sababu idadi yao ni ndogo na vizingiti kadha vya kikatiba.
Kulingana na kipengee cha 152 cha Katiba, hoja ya kumwondoa afisini Waziri sharti iungwe mkono na angalau thuluthi moja ya wabunge, ambayo ni sawa na wabunge 177. Wabunge wanaounga Dkt Ruto mkono hawawezi kufikisha idadi hii.
Na kabla ya Spika wa Bunge kuidhinisha hoja kama hiyo, sharti mbunge aliyeidhamini aonyeshe namna waziri amekiuka Katiba, sheria husika au kutumia vibaya mamlaka ya afisi yake kufaa kuondolewa kazini.
Spika wa bunge la kitaifa Justin Muturi amewahi kutumia hitaji hilo la kikatiba kutupilia mbali hoja kadha za awali za kuwaondoa mamlakani waliokuwa mawaziri, Anne Waiguru (Ugatuzi), Profesa Jacob Kaimenyi (Elimu) na waziri wa Afya Sicily Kariuki mwaka 2018.
Rais Kenyatta pia ana uwezo wa kuwanyamazisha wabunge wandani wa Dkt Ruto kuwa kushinikiza kuondolewa kwa baadhi yao wanaoshikilia nyadhifa kuu bungeni.