Habari

Wabunge kutoka Kenya ni miongoni mwa waangalizi wa uchaguzi wa urais Amerika

November 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE watatu na seneta mmoja kutoka Kenya wataungana na waangalizi kutoka mataifa mengine ya kigeni kufuatilia jinsi uchaguzi wa urais nchini Amerika utakavyoendeshwa mnamo Jumanne Novemba 3, 2020.

Wanaisasa hao ambao tayari waliondoka nchini Jumapili kuenda Amerika ni Jeremiah Kioni (Mbunge wa Ndaragua) Otiende Amollo (Rarieda) Abdi Shurie (Balambala) na Seneta wa Kisumu Fred Outa.

Bw Kioni ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kusimamia Utekelezaji wa Katiba (CIOC) ilhali Bw Amollo ni Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Kisheria (JLAC).

Karani wa Bunge la Kitaifa Michael Sialai alisema kuwa wabunge hao wataungana na wawakilishi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kufuatilia uchaguzi wa urais wa Amerika.

“Wabunge hao wamealikwa rasmi pamoja na IEBC kuhudumu kama waangalizi katika uchaguzi wa urais wa Amerika ambao ufanyika kati ya Novemba 3 na Novemba 4. Watakaa nchini Amerika kwa siku tano,” akasema Bw Sialai.

Mnamo Jumapili asubuhi Bw Kioni alithitisha kuwa hangehudhuria mkutano wa Naivasha kujadili ripoti ya mpango wa maridhiano (BBI) kwa sababu ya shughuli hiyo.

“Sitahudhuria mkutano wa Naivasha kujadili muafaka kuhusu BBI kwa sababu ninasafiri kuenda Amerika kufuatilia uchaguzi wa urais wa Jumanne, Novemba 3, 2020,” akasema.

Uchaguzi huo ambao Rais Donald Trump wa chama tawala cha Republican anapambana na aliyekuwa Makamu wa Rais chini ya utawala wa Barack Obama ambaye ni mgombea Joe Biden, umevutia idadi kubwa ya wapigakura ikilinganishwa na uchaguzi wa 2016.

Kulingana na vyombo vya habari vya kigeni kufikia Jumamosi, Oktoba 31, 2020, jumla ya wapigakura 138 milioni walikuwa wamepiga kura mapema.

Idadi hii ni zaidi ya asilimia 65 ya wapigakura waliokuwa wamepiga kura mapema wakati kama huo kuelekea uchaguzi wa urais wa 2016.

Wasiwasi mwingi umegubika uchaguzi huo baada ya Trump kutisha kutokubali matokeo endapo atashindwa huku kura za maoni zikionyesha Biden akiwa kifua mbele.

Mgombeaji atahitajika kupata angalau kura 270 za wawakilishi (Electoral College Votes) kutangazwa mshindi huku majimbo ya Florida, Arizona na North Carolina yakitarajiwa kuamua mshindi.