Habari

Wabunge wamtaka Rais afute madeni ya wanaoandamwa na Helb

November 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MUUNGANO wa Wabunge Vijana (KYPA) wamemtaka Rais Uhuru Kenyatta afutilie mbali madeni ambayo baadhi ya wahitimu wa vyuo vikuu wanadaiwa na Bodi ya Kutoa Mikopo ya Kufadhili Elimu ya Juu (Helb).

Wakiongozwa na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, wanachama sita wa muungano huo pia walipinga tangazo la bodi hiyo kwamba hivi karibuni litachapisha majina na picha za jumla ya watu 85,000 ambao hawajalipa mikopo waliochukua pamoja na malimbikizi.

“Ikiwa serikali imekuwa ikifutulia mbali madeni ya shirika ndege la Kenya Airways, wakulima wa majani chai, kahawa na miwa, mbona isifutilie mbali madeni ya wanafunzi waliohitimu kutoka vyuo vikuu lakini hawana uwezo wa kulipa mkopo kutoka kwa bodi ya Helb kwa sababu hawana ajira. Tunataka Rais Kenyatta afutilie mbali madeni haya,” akasema Bw Owino kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge, Nairobi, Jumanne.

Aliakuwa ameandamana na wenzake, Didmus Barasa (Kimilili), Caleb Amisi (Saboti), Nixon Korir (Langata), Thaddeus Nzambia (Kilome) na Mbunge Maalum Gideon Keter ambaye ni mwenyekiti wa NYPA.

Bw Owino ambaye zamani alikuwa mwenyekiti wa Chama cha Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi alishangaa ni kwa nini wanafunzi wa vyuo vikuu walazimishwe kulipa mikopo waliopewa kufadhili mafunzo yao ilhali wanafunzi wa polisi na vikosi vingine vya usalama hufadhiliwa kwa mfuko wa umma.

“Kando na mafunzo yao kufadhiliwa kwa mfuko wa umma walinda usalama huajiriwa moja kwa moja. Na baada ya kuajiriwa hatujasikia wakiandamwa walipe pesa ambazo zilitumiwa kugharimia mafunzo yao. Mbona wanafunzi werevu waliotihimu kujiunga na vyuo vikuu waadhibiwe kiasi hiki?” akauliza mbunge huyo wa chama cha ODM.

Naye Bw Barasa alisema wao kama wabunge watafanya kila wawezalo huhakikisha kuwa Helb inasitisha mpango wa kuchapisha majina ya wale ambao hawajalipa mikopo yao magazeti.

“Hii ni sawa na kuwatia kitanza vijana hawa na kuwaharibia majina mbele ya asasi ambazo zinaweza kuwapa ajira. Kwa vile Katiba inasema ni wajibu wa serikali kugharimia masomo ya watu, ni wajibu wake pia kuhakikisha kuwa waliohitimu wanapata kazi,” akasema Bw Barasa.

Mbunge huyo wa Kimilili alimshauri Mkurugenzi Mkuu wa Helb kuanzisha mpango wa kushauriana na wale ambao hawajalipa madeni yao ili afahamu ni kwa nini hawajalipa.

“Huu mpango wa kuchapisha majina yao magazetini haufai hata kidogo,” akasema.

Akaongeza: “Sharti tutafute njia za kuwawezesha waliopata mikopo ya Helb kuweza kulipa mikopo hiyo. Kwanza, serikali iwape ajira. Na pili, bunge hili litenge pesa katika bajeti ya kitaifa ili kulipia madeni hayo kama linavyofanya kwa madeni ya wakulima wa chai, kahawa na hata miwa.”

Wabunge hao pia walilalamikia faini za Sh5,000 kila mwezi ambazo Helb hutoza wale waliofeli kulipa madeni wakisema faini hiyo ni dhalimu.

Vilevile, wanataka Helb iondoe riba ya asilimia nne ambayo hutoza wahitimu kwa mikopo ili wapate kufadhili masomo yao.