Habari

Wabunge wataka amri ya kafyu isiwaguse

April 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE sasa wanataka wajumuishwe kwenye orodha ya wafanyakazi wa kutoa hudumu muhimu, wakilalama kuwa polisi wamekuwa wakiwadhulumu nyakati za kafyu.

Walisema wanatekeleza wajibu muhimu katika vita dhidi ya kuenea kwa virusi vya corona.

Suala hilo liliibuliwa katika kikao cha Jumatano na Mbunge wa Kandara Alice Wahome ambaye alilalamika kuwa Mbunge Mwakilishi wa Wanawake Laikipia Catherine Waruguru juzi alidhulumiwa na polisi baada ya kuwa nje dakika chache baada saa za kafyu kuanza.

Serikali imekuwa ikitekeleza amri ya kutotoka nje kuanzia saa moja usiku hadi saa kumi na moja alfajiri kuanzia Machi.

“Siku mbili zilizopita, Mheshimwa Waruguru ambaye ana mtoto mchanga alizuiliwa na polisi kwa saa mbili eti kwa sababu alikuwa nje dakika chache baada ya saa za kafyu kuanza. Nadhani suala hili linafaa kuangaliwa upya,” akasema.

Kauli yake iliungwa mkono na Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria ambaye alisema wabunge wamekuwa wakiteswa kwa sababu wameachwa nje ya orodha ya wanaotoa huduma muhimu ilhali huduma yao ni ya kimsingi.

“Mke wangu pia juzi alidhulumiwa katika kizuizi chicho hicho katika barabara kuu ya Thika ambako mheshimwia Waruguru alisumbuliwa,” akasema Bw Kuria.

Akaongeza: “Ni makosa kwa mke wa Rais mtarajiwa kama mimi kusumbuliwa. Ikiwa mke wangu atadhulumiwa kiasi hicho, sembuse raia wa kawaida?”.

Mbunge wa Eldas Adan Keynan pia alikosoa wale ambao waliandaa orodha ya wafanyakazi wanaotoa huduma muhimu walifanya makosa kwa kuwaacha nje.

“Haikuwa sawa kwa maafisa hao kutuacha nje. Tunatekeleza wajibu muhimu katika utawala wa taifa hili. Wabunge wanafaa kujumuishwa katika orodha ya wanaotoa hudumu muhimu. Hii ndio njia ya kipekee ya kutukinga dhidi ya mahangaiko tunayopitia sasa, mikononi mwa polisi,” Bw Keynan akasema.

Kulingana na orodha iliyotolewa na afisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai, wanahabari, wahudumu wa afya, walinda usalama ni miongoni mwa wafanyakazi wanaotoa huduma ya kimsingi na hivyo hawaathiriwi na amri ya kafyu.

Mnamo Jumamosi Rais Uhuru Kenyatta aliongeza muda wa kafyu kwa siku 21 zaidi sawa na amri ya kutoingia na kutotoka kaunti za Nairobi, Mombasa, Kilifi na Kwale.