Habari

Wabunge wataka kudhibiti mchakato wa uteuzi wa makamishna wa IEBC

August 21st, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE sasa wanapinga wazo la kujumuishwa kwa wawakilishi wa makundi ya kidini katika jopo ambalo litabuniwa kwa ajili ya kuteua makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Wakiongozwa na kiranja wa wachache Junet Mohamed na naibu wake Chris Wamalwa, wabunge hao badala yake wanataka wawakilishi wa vyama vya kisiasa wapewe nafasi kubwa katika jopo hili ambalo litateua watakaojaza nafasi ya makamishna wanne waliojiuzulu 2018 na 2017.

Wanasiasa hao walikuwa wakitoa maoni yao Jumanne kuhusu Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya IEBC ambao unalenga kubuni jopo la kuhudumu la uteuzi wa makamishna wa IEBC.

Bw Mohamed na wenzake, walipinga kipengee cha mswada huo kinachowapa wawakilishi wa makundi ya kidini wajibu mkubwa katika jopo hilo, wakisema hamna uhakikisha kuwa watu hao hawataendeleza wajibu huo kwa mapendeleo.

“Viongozi wa kidini ndio walitupa makamishna wa sasa ambao walitenda makosa mengi katika uchaguzi uliopita. Nini kipya watatupa?” akauliza Bw Mohamed ambaye ni Mbunge wa Suna Mashariki (ODM).

Akaongeza: “Washikadau wakuu katika mchakato wa uchaguzi ni vyama vya kisiasa. Uchaguzi unafanywa kwa niaba yao na tume ya uchaguzi ndiyo inasimamia.”

Chini ya mswada huu uliodhaminiwa na Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Kikatiba (JLAC), watu wanne watateuliwa katika jopo hilo na Tume ya Huduma za Bunge (PSC) na watu saba watakaoteuliwna Tume ya Utumishi wa Umma pamoja na ile ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).

Naye Bw Wamalwa ambaye ni Mbunge wa Kiminini (Ford-Kenya) alipendekeza kuwa jopo la uteuzi wa makamishna wa IEBC linafaa kuteuliwa kwa kuzingatia mwongozo wa muungano wa vyama vya kisiasa vinavyowakilishwa bungeni (IPPG).

“Mfumo huu ndio ulitumiwa kuteua makamishna walioendeshwa uchaguzi mkuu wa 1997,” akasema Bw Wamalwa.

Naye Mbunge Maalumu Jenipher Shamalla alisema ni wanasiasa wala sio viongozi wa kidini wanaopaswa kuamua wale watakaoendesha tume ya IEBC.

“Makundi ya kidini na viongozi wao hawaathiriki moja kwa moja na matokeo ya uchaguzi. Kwa hivyo, hawafai kujumuishwa katika uteuzi wa jopo la uteuzi wa makamishna wa IEBC,” akasema Bi Shamalla.