Habari

Wabunge wataka Oburu azime joto ODM

Na DAVID MWERE January 6th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

BAADHI ya wabunge wa ODM wanaomba kiongozi wa chama hicho, Seneta Dkt Oburu Oginga, kuitisha vikao vya  kamati husika za chama ili kushughulikia migogoro ya uongozi inayozidi kutokota kufuatia kifo cha aliyekuwa kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Tangu kifo cha Bw Odinga mnamo Oktoba 15, 2025, chama kimekumbwa na migawanyiko ya ndani, hasa kuhusu iwapo ODM inafaa kuwa mgombea wake wa urais au kumuunga mkono mgombea mwingine katika Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Kwa sasa, ODM imegawanyika katika makundi mawili makuu: kundi linalounga mkono kuchaguliwa tena kwa Rais William Ruto, linaloongozwa na Mbunge wa Suna East Junet Mohamed na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga; na kundi jingine linalopinga msimamo huo, likiongozwa na Katibu Mkuu wa ODM na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna.

Mvutano huo umeendelea kushuhudiwa hadharani huku Bw Junet na Seneta Sifuna wakirushiana maneno makali kuhusu mwelekeo wa kisiasa wa chama kuelekea 2027.

Mnamo Jumatatu, wabunge watano wa ODM  Dkt Otiende Amollo (Rarieda), Millie Odhiambo (Suba North), Seneta Catherine Muma (aliyeteuliwa), John Ariko (Turkana South) na Tom Odege (Nyatike)  walimtaka Dkt Oburu kuingilia kati, wakihimiza Bw Junet na Seneta Sifuna kupunguza lugha kali wanayotumia hadharani.

Ombi lao lilijiri huku Mbunge wa Alego Usonga Samuel Atandi akiwashutumu baadhi ya wenzake kwa kutokuwa na msimamo na kumshambulia vikali Seneta Sifuna, akisema hakuwa chochote kabla ya ODM kumjenga na kuonya kuwa hafai kuwa chanzo cha kusambaratika kwa chama.

Wakizungumza katika mkutano na wanahabari katika majengo ya Bunge, wabunge hao watano walisema ODM inahitaji umoja kwa dharura badala ya makabiliano, wakisisitiza kuwa hawajaegemea upande wowote bali wanalenga uthabiti wa chama.

Akisoma taarifa yao, Dkt Amollo alionya kuwa vita vya ndani vinaweza kugharimu ODM ngome zake za jadi huku vyama vidogo vikichukua nafasi yake.

“Tunasikitishwa na taswira ambayo imejitokeza ndani ya chama chetu siku za karibuni,” alisema Dkt Amollo, akibainisha kuwa ODM bado ndicho chama kikubwa zaidi nchini na kwamba Bw Junet ni Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa.

“Kwa kuzingatia nyadhifa walizopewa, tunawasihi maafisa wa chama kama Seneta Sifuna na Junet Mohamed waache mashambulizi ya maneno hadharani na warejee mezani kwa mazungumzo ya ndani,” aliongeza.

Kwa sababu hiyo, alisema, wanamtaka kiongozi wa chama, Dkt Oburu Oginga, kuchukua hatua za haraka, kuitisha mkutano wa kamati za  chama na kurejesha imani ya umma kabla ODM haijaanza kupoteza wanachama