Wabunge watishia kumuadhibu Matiang'i
Na CHARLES WASONGA
KAMATI ya Bunge kuhusu Usalama imetishia kuanzisha mchakato wa kumwondoa afisini Waziri wa Masuala ya Ndani Fred Matiang’i kwa kukaidi mwaliko wake kujibu maswali kuhusu masuala kuhusu wizara yake.
Wanachama wa kamati hiyo Jumatano walilalamika kuwa Bw Matiang’i amekataa kufika mbele yake mara mbili kutoa maelezo kuhusu mzigo wa madeni katika Idara ya Magereza na kudorora kwa hali maisha ya wafungwa na askari wa magereza.
“Kwa kuwa Waziri Matiang’i amekataa kufika mbele yetu mara mbili, hatutakuwa na budi ila kuanzisha harakati ya kumwadhibu kwa mujibu wa Katiba ya Kenya na Sheria za bunge. Lakini kwanza tutamwamuru kufika mbele ya kamati hii juma lijalo,” mwenyekiti wa kamati hiyo Bw Paul Koinange akawaambia wanahabari jana katika majengo ya bunge.
Bw Koinange, ambaye ni Mbunge wa Kiambaa alieleza kuwa kamati yake ilikuwa imemwalika Dkt Matiang’i na Katibu wake anayesimamia magereza Zeinab Hussein, ili kuwaeleza ni kwa nini wadeni wa idara hiyo hawajalipwa ilhali idara hiyo ilitengewa fedha nyingi .
“Pia tunamtaka kuelezea ni kwa nini wafungwa wanakabiliwa na uhaba wa chakula na mahitaji mengine huku askari wakiishi katika mazingira mabovu ilhali kamati hii iliidhinisha mgao wa zaidi ya Sh25 bilioni kwa idara,” akaongeza.
Bw Koinange alisema wanachama wa Kamati hiyo juzi ilitembelea gereza la Eneo la Viwandani, Nairobi, ambapo aliwapata wafungwa wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula kando na kuishi katika mazingira machafu.
Kulingana na Bw Koinange hatua ya Dkt Matiang’i kukaidi mwaliko wa kamati hiyo inaashiria kuwa haheshimu kamati hiyo ambayo ina jukumu la kuchunguza utendekezi wa wizara yake.
Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma alisema kamati hiyo ina mamlaka chini ya kipengee cha 152 (6) cha Katiba kuanzisha shughuli ya kumwondoa afisini Dkt Matiang’I ikiwa ataendelea kukaidi mialiko yake.
“Matiang’i anapaswa kufahamu kwamba njia ya kipekee ya kuwajibikia wananchi ni kupitia kamati hii. Na ikiwa hataki kufanya hivyo, basi tuko na mamlaka kikatiba kuidhinisha kuondolewa kwake afisini,” akasema.
Naye Bw Didmus Barasa (Kimilili) alisema kuwa kamati hiyo pia ilipania kuchunguza sakati ya uagizaji wa helikopta za polisi ambapo inadai mabilioni ya fedha yaliibiwa.
Majuzi, Spika wa Bunge la Kitaifa Justini Muturi aliwasuta mawaziri ambao hukaidi mialiko ya kamati za bunge akisema afisi yake haitasita kuidhinisha kupigwa kalamu kwa mawaziri kama hao.
Bw Muturi alitoa onyo hilo baada ya wenyeviti wa kamati za bunge kulalamika hatua ya mawaziri kukataa kufukia mbele yao imekwamisha kazi yao ya kushughulikia maombi ya umma na kushughulikia maswali ya wabunge.
Aliwaambia wenyeviti wa kamati kukoma “kuwabembeleza” mawaziri wakaidi bali wamjulishe visa hivyo ili achukue akichukue hatua zinazohitajika.
“Tungetaka kuwaona wenyeviti wa kamati mbalimbali wakianza kutumia mamlaka yao lakini kwa kuzingatia sheria,” Bw Muturi akasema kwenye taarifa aliyosoma bungeni
Spika alisema amepokea barua kutoka kwa mwenyekiti wa Kamati ya Leba na Masilahi ya Kijamii Bw Ali Wario (Bura) kuhusu Waziri mmoja ambaye amekuwa akikataa kuheshimu mialiko kadhaa ya kamati hiyo.
Kamati hiyo hupiga msasa utendakazi wa Wizara ya Leba inayoongozwa na Waziri Ukur Yattani.
Kamati ya Spoti na Masuala ya Kitamaduni pia imekabiliwa na wakati mgumu katika uhusiano wake na Waziri wa Michezo Rashid Echesa ambaye amekuwa akikaidi mialiko ya kamati hiyo. Kwa mara kadhaa, mwenyekiti wa kamati hiyo Victor Munyaka amekuwa akilalamika kuwa Bw Echesa hajafika mbele ya kamati yake kujibu maswali kadhaa yakiwemo malalamishi ya Timu ya Kitaifa ya Wachezaji waliolemaa miguu na mikono.
Mapema mwezi huu Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu wa Pesa za Umma (CPAIC) ilimtoza faini ya Sh500,000 Gavana wa Nairobi Mike Sonko kwa kukaidi mialiko yake mara kadhaa.