Habari

Wachina wavamia Gikomba, Nyamakima na Kamukunji kuuza mitumba

June 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na EDWIN OKOTH

WAKENYA Jumatatu walipokea kwa ghadhabu habari za Wachina kuvamia masoko ya Gikomba, Nyamakima na Kamukunji jijini Nairobi na kuanza kufanya biashara sawa na zinazoendeshwa na wakazi wa jiji.

Raia hao wa China wamefungua maduka na kuleta ushindani mkubwa kwa Wakenya ambao sasa wanalia kuharibiwa biashara zao.

Wafanyibiashara Wakenya wanasema Wachina hao wameanza kudhibiti mfumo mzima wa biashara ya bidhaa kutoka China kuanzia kuingiza bidhaa hizo nchini, kuuza kwa jumla na hata rejereja.

Wafanyibiashara waliozungumza na gazeti la Business Daily walisema raia hao wa China pia wameanza kuingilia masoko yao nje ya Nairobi.

“Tumekuwa tukiuza bidhaa hata nje ya Nairobi katika miji kama Kisii na Eldoret. Lakini Wachina wamefika hata huko na kufungua maduka. Biashara yetu inaendelea kuharibika kila siku,” akaeleza Lydia Njeri, ambaye jirani yake katika soko la Gikomba kwenye jumba la Mumbai Building ni Mchina.

Uhusiano wa kibiashara kati ya Kenya na China unapendelea Wachina zaidi katika kila hali. Kwa mfano mwaka jana Kenya ilinunua bidhaa za jumla ya Sh371 bilioni kutoka China huku Kenya ikiuzia nchi hiyo bidhaa za Sh11 bilioni pekee.

Wachina walianza kufanya biashara nchini yapata miaka 20 iliyopita wakiuza bidhaa za jumla katika eneo la viwandani, lakini majuzi wameanza kuanza rejareja katika maeneo ya Luthuli Avenue, Hurlingam, Gikomba, Nyamakima, Kamukunji na masoko mengine ndani na nje ya Nairobi.

Wafanyibiashara wa Kenya wanasema hawawezi kushindana na Wachina kutokana na kuwa wana uwezo wa kuuza bidhaa zao kwa bei ya chini. Katika soko la Gikomba, wageni hao wanauza bidhaa kwa jumla na pia rejareja.

Gazeti la Business Daily lilipotembelea Gikomba lilipata Wachina wengi ambao hata hawajui kuzungumza Kiingereza na wameajiri Wachina kufanya kazi za kuweka rekodi, huku Wakenya wakipewa kazi za kubeba mizigo kwa mikokoteni.

Ushindani huu mara kwa mara unaishia kuwa kupigana baina ya Wachina na Wakenya. Kisa cha majuzi kilitokea mwezi jana katika soko la Nyamakima ambapo Mchina mmoja alimpiga kofi Mkenya, hali iliyozua sokomoko na kusababisha kuharibiwa kwa duka la mgeni huyo.

Kulingana na wafanyibiashara Wakenya, Serikali ya Jubilee imechangia kutwaliwa kwa biashara zao na Wachina. Wanasema marufuku ya majuzi kuhusu ya kuagiza bidhaa mseto kwenye kontena moja pamoja na kanuni kali za ukaguzi zinawapendelea Wachina.

Wanasema kampuni iliyopewa kandarasi na Shirika la Ubora wa Bidhaa (KEBS) kukagua bidhaa kabla ya kuondoka China, imeajiri raia wengi wa nchi hiyo ambao hucheleweshwa kimakusudi mizigo inayoagizwa na Wakenya.

Wafanyibiashara hao wa Kenya pia wanalaumu Serikali kwa kukosa kutekeleza kikamilifu sheria za uhamiaji, hali ambayo imefanya iwe rahisi kwa wageni kufanya kazi na biashara nchini.

Mkurugenzi wa Uhamiaji, Alexander Muteshi alilaumu sheria ya ushuru kwa hali ya Wachina kuingilia biashara ndogo ndogo za Wakenya.