Wadau wafokea vikali kanuni mpya za kudhibiti pombe wakisema zitawaharibia biashara
WADAU katika sekta ya pombe wamekosoa vikali mapendekezo mapya ya Mamlaka ya Kudhibiti Matumzi ya Dawa za Kulevya (Nacada) wakiyataja kuwa yaliyo na uwezo wa kusambaratisha biashara zao.
Wakizungumza wakati wa mkutano wa pamoja Nairobi, Mwenyekiti wa Shirikisho la Wamiliki Baa na Mikahawa Michael Muthami alisema kwamba mapendekezo ya Nacada hayana mashiko ya kisheria.
“Sijaona amri yoyote wala sheria ya kuhimili mapendekezo haya. Nacada haiwezi kuamka tu siku moja na kuanzisha kanuni mpya,” akasema Bw Muthami akiongeza kwamba tayari kuna sheria za kutosha kuhusu matumizi salama ya pombe ila kilichokosekana ni utekelezaji wake.
Miongoni mwa kanuni zilizopendekezwa na Nacada ni kukweza umri wa kunywa pombe kutoka 18 hadi 21, kuharamisha mauzo ya pombe karibu na shule, maeneo ya kuabudu na mitaani.
Lililoonekana kukera zaidi wasanii na watumbuizaji ni pendekezo kwamba wanamuziki na watu mashuhuri wasiruhusiwe kutangaza vileo, jambo ambalo litakatizia wasanii wengi mbinu ya kujikimu.
Kanuni hizo mpya ni sehemu ya mapendekezo yaliyoko katika sera mpya ya Kitaifa kuhusu Matumizi Mabaya ya Pombe na Mihadarati ya 2025.
Sera hiyo inalenga kudhibiti changamoto ya uraibu wa pombe na mihadarati ambayo imevuruga familia kadhaa na kupunguza kasi ya maendeleo kitaifa.
Kulingana na takwimu za hivi punde kutoka kwa Nacada, karibu asilimia 13 ya Wakenya wenye umri kati ya miaka 15 na 65 (karibu watu milioni 4.7 ) hunywa pombe.
Idadi kubwa wa waraibu wa vileo hivyo ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 18 na 24.
Ajabu ni kwamba karibu mwanafunzi mmoja kati ya 10 wanaosomea shule za upili walikubali kwa wamewahi kutumia pombe huku umri wa wanaotumia vileo kwa mara ya kwanza ukipungua kila mwaka.
Isitoshe, watoto wenye umri wa mwaka mdogo wa kati ya miaka sita na tisa pia wanashawishiwa kunywa pombe manyumbani mwao na majirani.
Kero la unywaji pombe na madhara yake ni wazi kote nchini; kuanzia mijini hadi mashambani.