Habari

Wafadhili wahepa Kenya

October 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

WAFADHILI wameanza kukwepa kukopesha Kenya huku serikali ikipuuza ushauri wa mashirika ya kifedha ulimwenguni kwamba madeni yake yanageuka kuwa hatari.

Hatua ya wafadhili inatokana na hofu kuwa huenda Kenya ikashindwa kulipa madeni yake yanayozidi kuongezeka kila mara.

Hatua hii ya wafadhili kufunga mifereji ya pesa imweka miradi ambayo serikali ilinuia kutekeleza kwa kutumia mikopo katika hatari ya kukwama.

Hofu hiyo ya Kenya kulemewa na madeni ndiyo imefanya kampuni maarufu ya Amerika ya Bechtel kusimamisha kuanza ujenzi wa barabara kuu ya moja kwa moja kutoka Nairobi hadi Mombasa.

Kulingana na balozi wa Amerika nchini, Kyle Maccarter, deni la Kenya limefikia kiwango cha kutisha na japo kampuni ya Bechtel haijasitisha mradi huo, Amerika inataka kufanya biashara na Kenya kwa uwazi.

Kwenye mahojiano na gazeti la ‘Daily Nation’, balozi huyo alisema kwamba Amerika haitaki kuongezea Wakenya mzigo wa madeni.

“Deni la Kenya limefikia kiwango cha juu na ni jukumu lake kulipunguza,” akasema balozi huyo.

Deni la Kenya ni Sh6 trilioni ikiwa ni asilimia 63 ya utajiri wote wa nchi.

Hii inamaanisha kuwa madeni ya Kenya ni zaidi ya nusu ya uwezo wake wa kiuchumi na imepita kiwango kilichowekwa na mashirika ya kifedha ulimwenguni cha asilimia 50 ya utajiri wa nchini.

Waziri wa uchukuzi James Macharia alikiri kwamba mradi huo ulisimamishwa kwa muda kutokana na madeni ya nchi.

Kulingana na waziri huyo, baraza la mawaziri lilisimamisha ujenzi wa barabara hiyo kwa miaka miwili ili kuruhusu deni la Kenya kushuka.

Awali serikali ya China ilibadilisha uamuzi wa kufadhili awamu ya pili ya reli ya kisasa (SGR) kutoka Naivasha hadi Kisumu ikihofia kuwa Kenya haina uwezo wa kulipa deni hilo.

Kenya ilikuwa imeomba mkopo wa Sh350 bilioni kujenga reli ya kisasa hadi Kisumu lakini ikaamua kukarabati ya zamani baada ya China kukataa kuipatia mkopo huo.

Kulingana na mtaalamu wa uchumi John Mutua, China ilikataa mkopo huo kwa sababu mradi huo haungeweza kuleta faida.

Benki ya Dunia yaonya

Septemba 2019 Benki ya Dunia ilionya wafadhili kuwa Kenya inaweza kushindwa kulipa madeni yake baada ya kupitisha kiwango kinachopendekezwa.

Benki hiyo ilisema madeni ya Kenya yanaongezeka huku mapato yake yakiendelea kupungua.

Onyo hili linamaanisha kuwa wafadhili zaidi wataingiwa na baridi ya kupatia Kenya mikopo jambo linaloweza kufanya miradi mingi iliyoanzishwa na serikali ya Jubilee kukwama.

Mwezi huu Oktoba bunge la kitaifa lilifungulia serikali milango ya kuendelea kukopa lilipokubali ombi la Wizara ya Fedha la kukopa hadi Sh9 trilioni.

Wataalamu wa uchumi wanasema kwamba wafadhili wakikataa kupatia Kenya mikopo zaidi, serikali italazimika kukopa kutoka mashirika ya kifedha ya humu nchini hatua ambayo itaathiri uchumi.

Kufikia sasa, serikali imekopa Sh2.8 trilioni kutoka mashirika ya kifedha ya humu nchini na Sh3.7 trilioni kutoka nje ya nchi hasa kutoka China.

Mapema wiki hii, Kaimu Waziri wa Fedha, Ukur Yatani alisema Kenya imefilisika na hivyo italazimika kukopa zaidi ili kulipa madeni na kuendesha shughuli zake.