Habari

Wafanyakazi 28 wa kike wahitimu na kupokezwa vyeti vya uongozi sekta ya huduma ya maji

February 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na PAULINE ONGAJI

WAFANYAKAZI 28 wa kike wanaohudumu katika sekta ya huduma ya maji na usafi walihitimu na kupokezwa vyeti vya uongozi katika sherehe iliyofanyika Ijumaa katika katika hoteli ya Radisson Blu jijini Nairobi.

Mradi huo uliofadhiliwa na Benki ya Dunia ulihusisha washiriki kutoka maeneo ya Pwani na Kaskazini Mashariki ambapo washiriki walihitimu baada ya kusomea kozi ya miezi sita katika masuala ya uongozi wa huduma katika sekta mbali mbali za maji na usafi.

Akizungumza katika hafla hiyo, msimamizi wa utendaji wa Benki ya Dunia nchini, Camille Lampart, alisema kwamba mashirika mema ni yale yanayotoa mazingira yanayowawezesha wafanyakazi wake kuonyesha uwezo wao kikazi.

Kwa upande wake, Dkt Patricia Murugami, mwanzilishi na afisa mkuu mtendaji wa Breakthrough Leadership Transformation Group ambalo pia lilihusika katika maandilizi ya kozi hii, alisema kwamba mradi huu umewaruhusu washiriki kutambua uwezo wao wa uongozi, vile vile vipaji vyao.

Mwasisi na Afisa Mkuu Mtendaji wa Breakthrough Leadership Transformation Group Dkt Patricia Murugami azungumza katika hafla ya kufuzu kwa Wanawake  katika Sekta ya Huduma ya Maji na Usafi iliyoandaliwa hotelini Radisson Blu, Februari 21, 2020. Picha/ Kanyiri Wahito

Sababu ya kuhusisha washiriki kutoka maeneo haya ni kutokana na kuwa mradi wa ustawi wa maji na usafi uko katika sehemu hizi. Aidha, ushiriki wa wanawake kutoka maeneo haya kwenye uongozi katika sekta ya maji na usafi ni duni ilhali ni wao wanaoathirika pakubwa.

Kulingana na ripoti ya Benki ya Dunia kwa jina ‘Women in Water Utilities, Breaking Barriers Report’ kuongeza usawa wa kijinsia katika sekta ya maji kunaweza thibitisha matumizi ya maji, utendakazi wa kifedha, kiwango cha ubunifu na mahusiano ya wateja miongoni mwa mambo mengine.

Mwasisi na Afisa Mkuu Mtendaji wa Breakthrough Leadership Transformation Group Dkt Patricia Murugami (kulia) ashika cheti pamoja na mhitimu Fatuma Mwidadi katika hafla ya kufuzu kwa Wanawake  katika Sekta ya Huduma ya Maji na Usafi iliyoandaliwa hotelini Radisson Blu, Februari 21, 2020. Picha/ Kanyiri Wahito

Huu ni mradi wa kwanza wa mafunzo katika sekta ya maji ambapo wakurugenzi wasimamizi katika mashirika husika waliwateua wanawake watatu katika viwango tofauti kazini.

Mradi huu unanuiwa kuthibitisha uwezo wa uongozi miongoni mwa wanawake wanohudumu katika sekta za maji na usafi.