Wahitimu wa ualimu wahimizwa wawe wabunifu
Na LAWRENCE ONGARO
WALIMU wanastahili kulipwa mshahara mzuri ili kuwapa motisha kufanya kazi vyema.
Mbunge wa Thika, Mhandisi Patrick ‘Jungle’ Wainaina ametaja kazi hiyo kama ya heshima kubwa na kwamba wanafaa kutambuliwa.
“Nchi za ng’ambo taaluma za elimu na walinda usalama linaheshimiwa kikamilifu na ndiposa raia wa nchi hizo wanaheshima pakubwa na idara hizo mbili,” amesema Bw Wainaina.
Ameyasema hayo leo Ijumaa katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha St John Kilimambogo, Thika Mashariki.
Amwsema viwango vya ujuzi wa walimu vinastahili kuzingatiwa kwa minajili ya kuwapa mshahara wa kuridhisha.
Amesema atawasilisha mswada bungeni kuona ya kwamba pesa za nyumba kwa walimu unachunguzwa upya.
Ametoa mwito kwa wahitimu wapatao 490 kuwa dunia ya sasa ina ushindani mkali na kwa hivyo kila mmoja sharti awe na ubunifu wa kipekee.
“Siku hizi kupata ajira sio rahisi na kwa hivyo hatua ya haraka kuchukua ni kuwa na maono zaidi na kubuni mambo mapya,” amesema Bw Wainaina.
Wanafunzi watatu waliofanya vyema zaidi na kupata alama za juu zaidi ni Murigi Samuel Kibandi, Njau Denis Iregi, na Njuguna Jane Wambui.
Alisema lengo lake ni kuona ya kwamba shule nyingi za msingi zinafanyiwa ukarabati na kuzigeuza kuwa za kisasa.
“Ninataka kuona msingi wa elimu unapaliliwa kutoka chini kuelekea juu. Nitahakikisha kila mwanafunzi anapokea fedha za CDF bila kubagua,” alisema Bw Wainaina.
Mwalimu mkuu wa chuo hicho Bi Damaris Mbogo Mwea amewahimiza wahitimu hao wawe mabalozi wema wa kutegemewa.
“Ni lazima mfahamu kuwa maisha kule nje ni magumu. Kwa hivyo, kila mmoja wenu sharti awe na nidhamu wakati wowote. Alisema kupitia mtihani pekee sio kigezo cha kufanikiwa katika maisha lakini maadili na tabia njema ndiyo jawabu la maisha mema. Wewe kama mwalimu unastahili kuweka maadili mema kwa umma na ndiyo maana mtakuwa kama mfano wa kuigwa na wengi,” alisema Bi Mwea.