Habari

Wahudumu watatu wa mochari ya Mbagathi kizimbani kwa kuhadaa polisi

Na RICHARD MUNGUTI February 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MSIMAMIZI na wahudumu wawili wa mochari ya hospitali ya Mbagathi Level 5 jijini Nairobi wameshtakiwa kwa kutoa taarifa za uongo kwa afisa wa polisi kuhusu mtu aliyefariki.

Msimamizi Mkuu Jackline Njagi Wangithi, Karani wa Data Jackline Akoth Owino na Elizabeth Aoga walikana mashtaka matatu ya kutoa habari za uongo, njama ya kutekeleza uhalifu na kudai pesa kwa vitisho.

Wakiwa mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Milimani Ben Mark Ekhubi mnamo Ijumaa, watatu hao walikana kumfahamisha Konstebo Joseph Ogalo kwamba hawakuwa wameruhusu mwili wa James Mbugua uondolewe katika mochari ya Mbagathi Farewell Home.

Mwendesha Mashtaka wa Serikali Sonia Njoki alieleza korti kuwa watatu hao walimpa afisa huyo wa polisi habari kuhusu mtu mwingine wakijua ni za uongo.

Pia walikana kumuitisha Ann Mbugua Sh 30,000 mnamo Desemba 5, 2024 kwa nia ya kumlaghai.

Vile vile, walishtakiwa kwa kula njama ya kupata pesa kwa njia laghai kutoka kwa Bi Mbugua wakidai pesa hizo zilinuiwa kufuta bili ya hospitali ya James Mbugua.

Watatu hao waliachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu Sh100,000.