Habari

Waiguru nje! Aje?

June 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na MWANGI MUIRURI

HATUA ya Bunge la Kaunti ya Kirinyaga kupitisha hoja ya kumng’atua gavana Anne Waiguru imewaacha wengi wakijiuliza kulienda vipi ushawishi alio nao hadi Ikulu na makao makuu ya Jubilee ukashindwa kumwokoa.

“Sio siri kuwa Bi Waiguru ni mmoja wa wandani wa Uhuru katika siasa za eneo la Mlima Kenya, na ndiposa ndiye amekabidhiwa jukumu la kushirikisha BBI katika eneo la Kati. Lakini katika siasa hizi za kumng’atua, yaonekana amesalitiwa na chama cha Jubilee na hata Ikulu,” aliyekuwa mpinzani wake katika uchaguzi wa 2017, Bi Martha Karua aliambia Taifa Leo jana Jumanne.

Bi Waiguru ndiye mteule wa Rais Uhuru Kenyatta katika kuongoza harakati za Mpango wa Maridhiano (BBI) kanda ya Kati mwa nchi.

Mnamo Aprili madiwani walipojaribu kujadili hoja ya kumng’oa Bi Waiguru, Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju aliwaagiza wakome, na hata akamwondoa Kiongozi wa Wengi, James Murango katika wadhifa huo kama adhabu kwa jaribio la kuwasilisha hoja hiyo.

Hata miito ya mwenyekiti wa Jubilee katika Kaunti ya Kirinyaga, Muriithi Kang’ara kuwa wawakilishi 11 wa kuteuliwa walazimishwe kusimama na Bi Waiguru la sivyo watimuliwe haikufaa lolote.

Kwenye hoja ya Jumanne, madiwani 23 katika bunge hilo lenye jumla ya wawakilishi 33 walipiga kura ya kumtimua, wanne wakasusia huku sita wakikosa kufika bungeni.

Baadhi ya wanaotajwa kuhusika kwenye njama hiyo ni Katibu wa Wizara ya Usalama Dkt Karanja Kibicho, Naibu Gavana Peter Ndambiri na Mwakilishi wa Wanawake Wangui Ngirichi.

Ingawa Dkt Kibicho aliambia Taifa Leo jana Jumanne kuwa hahusiki na siasa za Kirinyaga, kauli iliyofuata iliashiria mengi: “Mimi ni mzaliwa wa Kaunti ya Kirinyaga aliye na haki ya kushiriki maamuzi ya kiutawala.”

Duru zinaeleza kuwa Dkt Kibicho ndiye pekee angeweza kufanikiwa kuhangaisha Bi Waiguru kutokana na mamlaka yake yanayotokana na cheo chake kikuu serikalini, na ushawishi mkubwa alio nao hadi ngazi ya Ikulu.

Kwa upande wake Bi Waiguru siku za majuzi amekuwa akiwataja wandani wa Naibu wa Rais William Ruto kama kiini cha masaibu yake kisiasa.

Kati ya wale ametaja ni aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri, Mbunge wa Gatundu ya Kati Moses Kuria na Bi Ngirichi.

Pia amekuwa akimlaumu naibu wake Bw Ndambiri kuwa aliyekuwa akitumiwa na wapinzani.

Lakini kuhusishwa kwa Dkt Kibicho pamoja na Dkt Ruto kwa pamoja katika masaibu ya Bi Waiguru kumezua hali tatanishi, ikizingatiwa kuwa wawili hawapatani kisiasa.

“Ingekuwa ni mrengo wa Dkt Ruto ambao umehusika, basi kungezuka mikakati ya kumkinga kutoka Ikulu na Jubilee asing’atuliwe. Hapo kwa Kibicho kuhusika ndiko kunaonekana kiini cha harakati hizo kwa kuwa kiutawala, Kibicho yuko karibu na Rais kumliko Waiguru,” asema Samuel Maina, ambaye alikuwa mwenyekiti wa wagombeaji viti wa Jubilee eneo la Mlima Kenya mnamo 2017.

Hapo jana, Bw Kiunjuri alipuzilia mbali madai ya Bi Waiguru kuwa alihusika: “Mimi sikuonekana ndani ya bunge la Kirinyaga nikijadili au kupiga kura.”

Naye Bw Kuria alisema: “Acha apambane na hali yake, na ajue sheria imelipatia bunge la kaunti mamlaka ya kumng’atua wala sio wabunge au wapiga kura wa Gatundu Kusini waliomtoa.”

Bw Ndambiri kwa upande wake alimlaumu Bi Waiguru kwa masaibu anayopitia.

“Tulijaribu kumnusuru Waiguru kutokana na masaibu haya, lakini akawa haambiliki wala hasemezeki. Alizusha kila aina ya vita na viongozi na wapiga kura wa Kirinyaga. Alipata ushauri usiofaa kutoka kwa wandani wake waliompotosha hadi akajihisi hagusiki,” akasema Ndambiri kwenye mahojiano jana.

Naibu huyo wa Bi Waiguru, ambaye atakuwa gavana kwa kipindi kilichosalia iwapo atabanduliwa, alisema kuwa kupitishwa kwa kura hiyo ya kumng’atua mkubwa wake ni matokeo ya kukataa kuwasikiza viongozi na wakazi wa Kirinyaga.

Mambo yalianza kuonekana kuwa telezi kwa Bi Waiguru wakati hata wabunge wa kaunti hiyo walipojitenga na suala hilo, wakisema bunge la kaunti kisheria liko huru kumulika utenda kazi wa afisi ya gavana.

Wabunge hao Bi Ngirichi, John Wambugu (Kirinyaga ya Kati), Gichimu Githinji (Gichugu), Kabinga wa Thayu (Mwea) na George Kariuki (Ndia) walisema hawakuwa na uwezo wa kuingilia hoja hiyo ya kumng’atua, wakisisitiza sheria ikubaliwe ifuate mkondo wake.

Baada ya hoja ya kumwondoa kupitishwa, Bi Waiguru alipuuza mbali hatua hiyo akiapa kwenda mahakamani. Alisema kuna agizo la mahakama kuwa hoja hiyo isijadiliwe na kwa hivyo uamuzi huo hauna maana yoyote.

Mnamo Aprili 7, 2020, Bi Waiguru alipata afueni Jaji Weldon Korir ailiposimamisha kwa muda kujadiliwa kwa hoja hiyo, kwa msingi kuwa janga la corona lilikuwa limesababisha kusimamishwa kwa mikutano yote ya halaiki hata ile ya kisiasa.