Waislamu watishia kujitenga na mfumo wa kisheria wa Kenya iwapo hukumu ya urithi haitafutwa
VIONGOZI wa Kiislamu wameonya kwamba huenda jamii yao itajitenga na mfumo wa kisheria wa Kenya iwapo serikali haitachukua hatua ya kufuta au kurekebisha hukumu ya Mahakama ya Juu kuhusu haki ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa kurithi mali.
Wakizungumza mjini Mombasa, wakiongozwa na Sheikh Abu Katada, walitaja hukumu hiyo kuwa “kisingizio cha kuvunja misingi ya sheria ya Kiislamu” na kudhalilisha mamlaka ya afisi ya Kadhi Mkuu.
“Hii ni njama fiche ya kuidhoofisha afisi ya Kadhi Mkuu. Sheria ya Kiislamu imeweka wazi masuala ya urithi. Mambo haya hayawezi kuamuliwa na mahakama ya kidunia.
Ikiwa serikali itazidi kupuuza misimamo ya dini yetu, basi tutalazimika kuanzisha utawala wetu wa Kiislamu,” Bw Athman Shariff alionya.
Kulingana na viongozi hao, Katiba ya Kenya imeipa afisi ya Kadhi Mkuu mamlaka ya kuamua masuala ya ndoa, talaka na urithi kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu, lakini hukumu hiyo ya Mahakama ya Juu ni kinyume na hayo.

“Ndio, mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa ana haki ya kulelewa, kusomeshwa na kupendwa. Lakini si haki ya kurithi mali kwa mujibu wa dini yetu. Hii hukumu inakiuka mafundisho ya Kiislamu na inaleta choko choko miongoni mwa waumini wetu,” alisema Sheikh Katada.
Bw Shariff, mtaalamu wa sheria za Kiislamu, alidai kuwa kuna mpango maalum wa kuondoa kabisa mamlaka ya Kadhi Mkuu.
“Wameanza na urithi. Kesho wataingia kwa ndoa na talaka. Afisi hii inapaswa kuheshimiwa kama taasisi ya kikatiba. Ikiwa tutaendelea kupuuzwa, basi hatutasita kuanzisha jimbo la Kiislamu,” aliongeza Bw Shariff.
Viongozi hao pia waliwalaumu wanasiasa wa Kiislamu kwa kimya chao wakisema wamewasaliti waumini kwa kutanguliza maslahi yao binafsi.
“Wako wapi magavana, wabunge, wawakilishi wa wanawake na mawaziri wa Kiislamu? Hamuwezi kuja kwa Waislamu wakati wa kura pekee. Simameni sasa na dini yenu,” alisisitiza Bw Mohamed Abubakar.
Aidha, walimtaka Rais William Ruto kuingilia kati mzozo huu akisema amekuwa na historia ya kuwapa Waislamu nafasi serikalini, lakini ni lazima pia alinde imani yao.
Walisema hatua ya kujenga kanisa la Sh1.2 bilioni katika Ikulu ni ishara kuwa serikali inakumbatia dini moja huku ikipuuza nyingine. Wakamtaka Rais ajenge pia msikiti wa hadhi sawa na huo.
“Kenya si nchi ya Kikristo wala ya Kiislamu. Tumeishi kwa amani na dini zote kwa miaka mingi. Tunachotaka ni usawa na kuheshimiwa kwa mafundisho ya dini yetu,” alisema Sheikh Katada.
Viongozi hao walitangaza kuanza mchakato wa kukusanya sahihi milioni moja kupinga rasmi hukumu hiyo, na pia kuwasilisha ombi la mapitio ya hukumu kupitia kwa wanasheria wa Kiislamu.
“Tuna wanasheria wetu na wataalamu wa dini. Tutasimama imara hadi haki ya Waislamu iheshimiwe,” walisema kwa kauli moja.