Waititu amshtaki Ngilu kwa dai la kueneza chuki
Na RICHARD MUNGUTI
Kwa ufupi:
- Bw Waititu anaomba mahakama kuu imzuie Bi Ngilu kueneza chuki na kusababisha hali ya taharuki
- Wakazi wa Kiambu walikuwa wanaomba hatua uchukuliwe dhidi ya Bi Ngilu
- Bi Ngilu alisema marufuku hiyo ya makaa na usombaji changarawe itadumu
GAVANA wa Kiambu Bw Ferdinard Waititu jana alimshtaki Gavana Charity Kaluki Ngilu kwa matamshi ya uchochezi kuhusu biashara ya makaa.
Katika kesi hiyo dhidi ya Bi Ngilu, Bw Waititu alisema kumekuwa na uhasama mkali baina ya wakazi wa kaunti hizi mbili
Bw Waititu anaomba mahakama kuu imzuie Bi Ngilu kueneza chuki na kusababisha hali ya taharuki kati ya wakazi wa kaunti ya Kitui na wafanyabiashara wa makaa.
Gavana huyu amesema uhusiano kati ya kaunti za Kiambu na Kitui umedorora.
“Naomba hii mahakama imzuie Bi Ngilu kutoa matamshi ambayo yanaweza kuibua hisia za chuki na uchochezi baina ya wakazi wa kaunti hizi ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikishirikiana na kufanya biashara mbalimbali,” alisema Bw Waititu katika kesi aliyowasilisha katika Mahakama Kuu jana.
Gavana huyu wa Kiambu amesema mnano Feburuari 2018 Bi Ngilu alitoa matamshi kwamba uchomaji makaa umepigwa marufu.
Bw Waititu alisema kuwa tangu matamshi hayo yatolewe kumekuwa na kisa ambapo lori la kusafirisha bidhaa liliteketezwa katika kaunti ya Kitui.
Kutokana na visa hivyo vya uteketezaji magari ya kusafirisha makaa, wakazi wa Kiambu waliandamana na kusababisha msongamano mkubwa wa magari katika barabara ya Nairobi- Busia.
Wakati wa kisa hicho magurudumu ya magari ya watu yalitolewa pumzi na kuzua hali ya taharuki. Kwa muda wa jumla ya saa nane, hali ilikuwa si hali kwenye barabara hiyo.
Wakazi wa Kiambu walikuwa wanaomba hatua uchukuliwe dhidi ya Bi Ngilu.
Kufuatia matamshi hayo Bi Ngilu aliagizwa afike mbele ya tume ya kitaifa ya utangamano na uuwiano kuandikisha taarifa kuhusu matamshi hayo.
Marufuku haitajadiliwa
Ijumaa baada ya ushindi wa Bi Ngilu wa Agosti 8 2017 kuthibitishwa na Mahakama kuu ya Milimani Nairobi, akiwahutubia wafuasi wake na wakazi wa Kitui waliofika kufuata uamuzi , gavana huyu alisema , “marufuku ya uchomaji makaa hayatajadiliwa tena. Hakuna kuchoma makaa na hakuna kupitisha makaa katika kaunti ya Kitui.”
Bi Ngilu alisema marufuku hiyo ya makaa na usombaji changarawe itadumu.
“Kaunti ya Kitui imegeuzwa kuwa jangwa. Miti asili yote imekatwa na kuchomwa makaa na wafanyabiashara kutoka kaunti nyingine. Marufuku haya yatadumu,” alisema Bi Ngilu huku akishangiliwa.
Bw Waititu anaomba mahakama iratibishe kesi aliyomshtakiwa Bi Ngilu kuwa ya dharura.