Habari

Waititu, mkewe wanavyokodolea macho maisha ya jela kwa kutafuna Sh588m za kaunti

Na RICHARD MUNGUTI February 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

ALIYEKUWA Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu, mkewe Susan Wangari na washtakiwa wengine wawili wanakodolea jela macho baada ya kupatikana na hatia kushiriki ufisadi wa Sh588 milioni na matumizi mabaya ya mamlaka.

Waititu, mkewe Susan, Charles Chege na mkewe Beth Wangeci pamoja na aliyekuwa waziri wa barabara Luka Mwangi Wahinya watajua hatma yao Alhamisi wakati mahakama itakapopitisha hukumu.

Waititu na mkewe Susan, Chege na mkewe Beth huenda hawatasherehekea Valentino pamoja kwa sababu huenda watakuwa wamehukumiwa vifungo vya gerezani.

Waititu ndiye gavana wa pili kufungwa kwa ulaghai wa fedha za umma.

Wa kwanza kufungwa jela miaka minne alikuwa Gavana wa Samburu Moses Lenolkulal mwaka jana kwa hatia ya kutia kibindoni zaidi ya Sh80 milioni.

Wakili wa Waititu John Swaka aliomba mahakama isimsukumie kifungo cha jela akisema ni mgonjwa na wa umri mkubwa.

Wakili mwingine Jeremiah Njenga aliomba washtakiwa wenza wa Waititu wahurumiwe.

Lakini upande wa mashtaka ulisema pesa za umma zilipotea na washtakiwa wanastahili kifungo cha gerezani sawia na faini.

Hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Milimani Bw Thomas Nzioki alisema Bw Waititu alipora na kubonda pesa za umma badala ya kuzitunza impasavyo mtumishi wa umma.

Bw Nzioki aliwapata na hatia Bw Waititu, Susan, mwanakandarasi Charles Chege na aliyekuwa waziri wa barabara kaunti ya Kiambu Luka Mwangi Waihinya na hatia ya kufuja Sh588,198,328.20.

Hakimu alisema kwamba Bw Chege na Bw Waititu walikuwa marafiki wa chanda na pete kumbe uhusiano wao “ulikuwa wa kufyoza pesa za umma.”

Mahakama ilisema upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa serikali Faith Mwila umethibitisha kesi dhidi ya wanne hao.

Bi Mwila aliwasilisha mashahidi 38 na stakabadhi 129 kuthibitisha kesi dhidi ya Waititu na wenzake.

Mashahidi waliambia mahakama TEL haikuwa imehitimu kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara iliyopewa kukarabati Thika, Juja, Limuru na Kiambu.

TEL haikuwa na maafisa waliohitimu na mmiliki wake Chege hakuwa amehitimu.

Chege alikuwa ameghushi vyeti vya uhadisi kutoka vyuo vikuu vya Nairobi (UoN) na Jomo Kenyatta (JKUAT).

Mahakama ilisema pia Chege alighushi stakabadhi za kufanya kazi kwa ushirikiano na kampuni ya Wachina ya China Wu Yi.

“TEL ilisaidiwa kwa njia ya ufisadi kushinda zabuni hiyo iliyokuwa inang’ang’aniwa na makampuni mengine manne,” alisema Bw Nzioki.

Hakimu aliendelea kusema kwamba ni wazi TEL ilishinda zabuni hiyo kwa njia ya ufisadi, “hivyo basi zabuni hiyo ilipotea kutoka mwanzo na kupelekea kupotea kwa pesa za umma zaidi ya Sh588 milioni.”

“Ushahidi uliowasilishwa mahakamani umethibitisha kwamba Bw Waititu aliruhusu pesa za umma zilizokuwa zimetegewa mradi wa ujenzi wa barabara zilipwe kampuni ambayo haikuwa imehitimu na hatimaye akapewa mgao wake.”

Bw Nzioki alisema katika uamuzi uliochukua masaa manne kusoma na kuchambua ushahidi kwamba upande wa mashtaka umethibitisha kabisa washtakiwa wako na hatia.

Mahakama ilimpata Bw Waititu na hatia ya kupokea Sh25milioni kutoka kwa kampuni ya Testimony Enterprise Limited (TEL) yake Bw Chege akijua pesa hizo zimepatikana kwa njia isiyo halali.

Hakimu alisema gavana huyo wa zamani alipokea Sh25,624,500 kutoka kwa Bw Chege akijua ni sehemu ya pesa Sh588 milioni zilizokuwa zimelipwa TEL kwa njia ya ufisadi.

Bw Waihinya alipatikana na hatia ya kuidhinisha TEL ilipwe Sh588 milioni akijua haijahitimu na haikuwa na wataalam wa kujenga barabara.

Bw Nzioki alitupilia mbali tetezi za Bw Waititu kwamba kesi hiyo ilikuwa ya kisiasa kwa vile alikuwa katika mrengo wa Tanga Tanga uliokuwa unampinga rais mstaafu Uhuru Kenyatta dhidi ya Rais William Ruto.

Bw Nzioki alisema “hakuna siasa katika kesi hii kamwe kwani mshtakiwa alipokea pesa za umma alizokuwa anapasa kulinda.”

Hakimu alisema ni wazi pesa zilitoka kwa akaunti za Kaunti na kulipwa TEL ambayo ilimpelekea Bw Waititu na kampuni zake Saika Two na Bienvenue Delta Hotel.

Washtakiwa hao wamepewa fursa ya kujitetea kabla ya kuhukumiwa.

Bw Waititu ameomba mahakama imwonee huruma akisema “anaugua na anahitaji madawa kila wakati.”

Hakimu aliamuru washtakiwa wazuiliwe rumande hadi Feburuari 13, 2025.