HabariHabari za KauntiHabari za Kitaifa

Wakazi jijini kujistarehesha Central Park korti ikiamuru ifunguliwe kwa msimu wa sikukuu

Na SAM KIPLAGAT December 16th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MAHAKAMA imeamuru bustani ya Central Park jijini Nairobi ifunguliwe kwa umma baada ya kufungwa kwa miaka mitatu.

Jaji wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi Anne Omollo alitoa uamuzi huo wa muda unaoshurutisha serikali ya Kaunti ya Nairobi kufungua bustani hiyo.

Bi Omollo hakuelewa sababu za kufungwa kwa eneo hilo msimu wa sherehe.

Bustani ya Central Park iko mkabala wa bustani ya Uhuru Park kwenye barabara ya Kenyatta Avenue. Inafahamika kwa mnara maarufu wa Nyayo – mkono wa aliyekuwa Rais Daniel Arap Moi.

Mnara wa Nyayo ulio katika bustani ya Central Park jijini Nairobi awali. PICHA | MAKTABA

Shirika la kimazingira la Green Belt Movement (GBM) lilipinga kufungwa kwa bustani za Uhuru Park na Central Park likisema kaunti haijabainisha kiini cha hatua hiyo licha ya kutumiwa barua ieleze sababu.

“Uamuzi ni kwamba washtakiwa (Kaunti ya Nairobi) wamekiuka haki za kikatiba za Wakenya kwa kukosa kutoa maelezo kwa mujibu wa Kifungu cha 35. Pia kukosa kueleza sababu ya Central Park kufungwa kwa muda mrefu tangu 2021 na ufunguzi wa mara kwa mara wa Uhuru Park,” Jaji Omollo alisema katika uamuzi wake wa muda kwenye kesi itakayosikizwa tena Februari 17, 2025.

Shirika la GBM lilifika kortini kukata rufaa dhidi ya hatua ya kufungwa kwa bustani ya Central Park, likisema ilikiuka haki za wakazi.

Lilihoji kwamba ni kwa sababu hiyo ambapo wakazi wameamua kutumia maeneo ya kibinafsi, yakiwemo makutano ya barabara, ili kujituliza.

Shirika hilo lililalamikia ukosefu wa maeneo mazuri ya kujivinjari.

Mwanamume akitulia katika mojawapo ya viti vilivyoko Central Park awali. PICHA | MAKTABA

Tukio la wakazi kujistarehesha katika mazingira hatari linadunisha hadhi ya binadamu huku serikali ikilaumiwa kwa ‘kulala kazini’.

“Central Park ilifungwa na ujenzi unaendelea bila dalili zozote kwamba itawahi kufunguliwa,” mwenyekiti wa GBM, Bi Nyaguthie Chege, alisema na kumshutumu Gavana Johnson Sakaja wa Nairobi kwamba licha ya kutoa ahadi nyingi Central Park bado haijafunguliwa.