Wakazi Mombasa wataka mitaa iliyo na visa vya Covid-19 inyunyuziwe dawa
Na MISHI GONGO
BAADHI ya wakazi mjini Mombasa sasa wanataka kaunti hiyo kuweka mpango wa kunyunyuzia sabuni na dawa ya kuua vini mara kwa mara katika mitaa iliyoandikisha idadi kubwa zaidi ya waliopata maambukizi ya virusi vya corona.
Kufikia Jumatano, Wizara ya Afya ilikuwa imerekodi visa 106 vya corona katika Kaunti ya Mombasa, huku eneobunge la Mvita likiongoza kwa maambukizi.
Visa vilivyorekodiwa ni kutoka mitaa ya Mji wa Kale, Ganjoni, Memon, Miritini, Mikindani, Kibokoni, Tudor, Mlaleo na Bamburi.
Walisema serikali ya kaunti ya Mombasa inafaa kunyunyuzia dawa katika Mji wa Kale, Kibokoni na maeneo yote yaliyo kitovu cha mji huo ili kudhibiti maambukizi zaidi.
Mfanyabiashara katika mji huo Bw Ali Said alisema maeneo hayo hutembelewa na watu wengi kutekeleza biashara na shughuli mbalimbali.
“Mjini ndipo kuna afisi zote za kaunti, biashara za kila aina ziko hapa, kunyunyuziwa dawa kutazuia watu kupata virusi hivyo,” akasema.
Mwingine Bw Yaqoub Ismail alisema wanahofia maambukizi kuongezeka hasa wakati huu wa Ramadhan ambapo watu wanazuru eneo la Kibokoni na Mji wa Kale kununua bidhaa mbalimbali zikiwemo chakula na nguo.
“Tunahofia kuongezeka kwa idadi ya maambukizi na hivyo tunaomba serikali kunyunyuzia dawa za kuuwa viini katika maeneo haya,” akasema.
Wakazi wa Mombasa hutegemea soko la Marikiti katika kununua bidhaa mbalimbali.
Hata hivyo, wafanyabiashara wengi katika eneo hilo, hawavalii maski na hukaa pamoja kuendeleza biashara zao bila kuzingatia hatari za kiafya zinazohusiana na matendo hayo.
Leo Alhamisi serikali ya kaunti hiyo imeanza shughuli ya kuwapima wakazi katika eneo la Mvita.
Afisa mkuu wa Afya katika kaunti ya Mombasa Aisha Abubakar, amesema hatua hiyo ni kugundua idadi kamili ya maambukizi ili kuchukua hatua muafaka kudhibiti kuenea zaidi kwa virusi hivyo.
“Watakaopatikana na virusi watawekwa katika mpango wa kushughulikia wagonjwa wa Covid-19 ili kuzuia kusambaa zaidi kwa ugonjwa huo,” amesema.
Mbunge wa Mvita Abdulswamad Sheriff Nassir amesema shughuli hiyo itaendelea hadi Jumatatu wiki ijayo kuhakikisha wakazi karibu wote katika eneo hilo wanajua hali zao.
Amewahimiza wakazi wa eneobunge la Mvita kujitokeza katika mchakato huo.
Gavana wa Mombasa Hassan Joho, alisisitiza kuwekwa marufuku ya kutoka nje kwa wakazi hao kwa muda.
Hata hivyo, Rais Uhuru Kenyatta alipinga hatua hiyo, akisema kuwa haitawezekana kuufunga mji huo.