Wakazi wa Gatundu wahakikishiwa usalama wao
Na LAWRENCE ONGARO
WAKAZI wa Gatundu Kusini wamepewa hakikisho kuwa usalama wao utaimarishwa na kuwa kama zamani.
Wiki moja iliyopita wahalifu walivamia kijiji cha Githioro Ichaweri na kumuua mkazi mmoja huku pia wakimnajisi mwanamke.
Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i alitoa hakikisho hilo Alhamisi alipozuru kijiji cha Rais Uhuru Kenyatta cha Mutomo.
Dkt Matiang’i alipozuru kijiji hicho aliwahutubia wakazi hao na kuwapa hakikisho kuwa maafisa wa usalama watafika hapo kwa fujo ili kukabiliana na visa vya utovu wa nidhamu na ukosefu wa usalama.
“Baada ya serikali kufanya uchunguzi wake kuhusu uvamizi huo, washukiwa wanne wametiwa nguvuni ambapo kwa sasa wanasaidia polisi katika uchunguzi,” alisema Dkt Matiang’i.
Aliwahimiza machifu na manaibu wao kushirikiana na wakazi wa kijiji hicho ili kuimarisha hali ya usalama.
Alisema serikali itafanya mabadiliko ya maafisa wa usalama ili usalama uimarike zaidi.
“Kuna maeneo kadha ambayo hayana machifu. Kwa hivyo, nafasi zao zitajazwa mara moja hivi karibuni ili pia kuimarisha usalama mashinani,” akasema.
Aliongeza kusema kuwa serikali haiwezi shindwa kuimarisha usalama, na kuongeza kuwa wakazi hao wataona mabadiliko.
” Kwanza ninaomba msamaha kwa niaba ya maafisa wa usalama kwa yale mlioyapitia majuzi. Nina wahakikishia usalama wenu kutoka leo. Ninajua leo mtalala na usalama bila tatizo,” aliwapa matumaini Dkt Matiang’ i.
Mbunge wa Gatundu Kusini Bw Moses Kuria alisema kiongozi yeyote anayechochea wananchi anastahili kuchukuliwa hatua za kisheria mara moja.
“Hatuwezi kukubali watu wachache kuchochea wananchi,” alisema Bw Kuria.
Wakazi wengi waliohojiwa walikiri kwamba kwa zaidi ya kipindi cha mwezi mmoja wahalifu wamewahangaisha kabisa.
Wakazi wengi walionyesha nyuso za huzuni wakati waziri Matiang’i alizuru kijiji hicho.
Kila chifu na naibu wake walihimizwa kufanya mikutano ya baraza ili kupata maoni ya wananchi na kuyatatua.
Aidha Matiang’i alisema yeye akiwa ndiye Waziri wa Usalama hatakubali watu wachache kuhangaisha raia na wakazi waadilifu.
“Serikali itawasaka popote pale walipo. Kwa hivyo, hata mkijificha tutawanasa,” alionya Dkt Matiang’i.
Wakati wa ziara hiyo Dkt Matiang’i aliandamana na mbunge wa Gatundu Kusini Bw Moses Kuria, wa Gatundu Kaskazini Bi Wanjiku Kibe, Mwakilishi wa Wanawake Bi Gathoni Wa Muchomba pamoja na maafisa wakuu wa usalama kutoka eneo la Kati wakiongozwa na Bw Wilfred Nyangwanga.
Alipokuwa akirejea Nairobi waziri alisimama kwa vituo kadha hasa Kamwangi na Igegania akihutubia wakazi hao waliofurahia kumwona na ambapo walimshangilia.