Wakazi wa Kiambu wafurahia Sensa ya 2019
Na LAWRENCE ONGARO
HUKU watu wengi wakilalamika kuhusu hesabu kamili ya sensa, iliyotangazwa na serikali, wakazi wengi wa Kaunti ya Kiambu wanaishabikia.
Mfanyabiashara mjini Thika, Bw Elius Ngaru Mwaura anasema matokeo hayo ya Kiambu yanaridhisha na kwa hivyo wanatarajia kupata mgao wa fedha ipasavyo.
Kwa mfano takwimu za sensa zinaeleza kuwa kaunti ndogo ya Ruiru ina idadi ya watu 371,111.
Thika Magharibi na Mashariki, ina watu 324,776. Halafu Juja inajivunia kuwa na watu jumla 300,949.
“Maeneo hayo matatu yanastahili kukatwa mara mbili kila moja ili yawe na uwakilishi ufaao wa uongozi,” alisema Bw Mwaura.
Alisema kulingana na jinsi mambo yalivyo, maeneo hayo yamepata idadi kubwa ya watu kwa sababu ya barabara kuu ya Thika Superhighway ambayo imesambaza hali ya biashara kwa maeneo mengi.
Wakati huo pia kuna vyuo vikuu kadha katika miji hiyo na kwa hivyo idadi ya watu ni ya juu.
“Hata ingawa mji wa Kiambu ndiyo makao makuu ya Kaunti ya Kiambu, ukweli wa mambo ni kwamba biashara kubwa na fedha za mapato nyingi zinatoka mjini Thika,” alisema Bw Mwaura.
Alisema ni wazi sasa kila eneo litapata mgao wake wa kifedha kulingana na jinsi idadi ya watu inavyoeleza.
Bw Daniel Mwangi ambaye ni Mfanyabiashara na pia mkazi wa Thika mjini alisema Jumanne kwamba ameridhishwa na matokeo hayo.
Alisema maeneo ya Thika na Ruiru yanastahili kukatwa mara mbili ili kupata uwakilishi unaofaa.
“Kwa mfano, miji ya Thika na Ruiru inahudumia watu wengi na biashara ni nyingi katika maeneo hayo,” alisema Bw Mwangi.
Kulingana na takwimu kamili zilizotolewa, Kaunti ya Kiambu ina idadi ya watu wapatao 2,417,735 milioni.
Maeneo mengine ni kaunti ndogo ya Gatundu Kaskazini 109,870. Gatundu Kusini 122,103. Githunguri ,165,232. Kabete 199,653. Kiambaa 236,400. Kiambu Mjini 145,903. Kikuyu 187,122. Lari 135,303 halafu Limuru ni 159,314.
Katika eneo pana la Kati, Kaunti ya Kiambu imezipiku kaunti kadha katika sehemu hiyo.
Kwa mfano, huku Kiambu ikiwa na watu 2,417,735 milioni, Nyeri ina 759,164. Kirinyaga ina 610,411. Halafu Nyandarua ina idadi ya watu 631,281.
Halafu inadaiwa kuwa idadi kubwa ya watu wanaoishi Kiambu wanafanya kazi jijini Nairobi na kwingineko. Wengine nao wamejinunulia vipande vvya ardhi huko kutoka kwingineko.