Habari

Wakenya wala nyama kwa wingi licha ya bei kupanda, ripoti yasema

Na PETER MBURU January 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

THAMANI ya nyama ambayo Wakenya hula ilipanda kwa kiwango kikubwa hadi Sh304.6 bilioni katika mwaka wa 2023, ishara kwamba wangali wanapenda kitoweo hicho licha ya bei yake kupanda kila mara.

Takwimu mpya zinaonyesha kuwa Wakenya walikula tani 556,653 za nyama mnamo 2023 ambayo inawakilisha ongezeko la asilimia 19.8 kutoka tani 464,512 ya nyama iliyozalishwa mnamo 2022.

Hii ndio ilikuwa mara ya kwanza ambapo thamani ya nyama inayozalishwa nchini kwa mwaka ilizidi Sh300 bilioni, huku bei ikipanda kwa asilimia 29 ndani ya miaka mitano.

“Jumla ya tani 556,653 za thamani ya Sh304.6 bilioni zilizalishwa mnamo 2023 ikilinganishwa na tani 464,512 ya nyama yenye thamani ya Sh240.7 bilioni mnamo 2022,” inasema ripoti ya Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) katika ripoti kuhusu Uzalishaji katika Sekta ya Kilimo Kitaifa, 2024.

Ripoti hiyo inasema kuwa thamani ya nyama iliyozalishwa nchini mnamo 2023 iliongezeka kwa kiwango cha asilimia 26.5.

Kulingana na ripoti hiyo, aina ya nyama iliyoliwa kwa wingi ni ile ya ng’ombe (ya thamani ya Sh129.5 bilioni), nyama ya mbuzi (Sh53.9 bilioni), nyama ya kuku (Sh34.7 bilioni), nyama ya kondoo (Sh34.2 bilioni), nyama ya ngamia (Sh32.5 bilioni) na nyama ya nguruwe (19.5 bilioni).

Nyama ya ng’ombe ndio ilizalishwa kwa wingi mnamo 2023, ikichangia asilimia 42.7 ya nyama yote iliyozalishwa mwaka huo.Inafuatwa na nyamba ya kuku ambayo ilichangia asilimia 16.8 ya nyama ambapo tani 93,622 zilizalishwa, kisha nyama ya mbuzi (tani 77,521), nyama ya ngamia (tani 55,204).

“Ulaji wa nyama nyekundu (ya ng’ombe, mbuzi, kundoo na ngamia) uliongezeka kwa kiwango cha asilimia 23.3 mnamo 2023 ikilinganishwa na mwaka wa 2022. Kwa upande mwingine ulaji wa nyama nyeupe (nyama ya nguruwe, kuku na sungura) uliongezeka kwa kiwango cha asilimia 10 katika kipindi sawa na hicho,” KNBS ilisema.

Thamani ya nyama inayozalishwa nchini inachangiwa na ongezeko la wanyama wanaochinjwa kwa ajili ya nyama na ongezeko la bei.Kwa wastani thamani ya tani moja ya nyama ni Sh547,260 mnamo 2023 ambayo iliongezeka kutoka Sh518,231 mnamo 2022.

Katika miaka ya hivi karibuni, bei ya nyama imeongezeka kutoka Sh423,023 kwa tani moja mnamo 2019.Idadi ya mifugo wanaochinjwa pia imeongezeka kutoka milioni 66.2 milioni mnamo 2020 hadi milioni 80 kufikia mwaka wa 2023.

Kuku ndio wamechinjwa kwa wingi zaidi. Ripoti ya KNBS inasema kuwa uzalishaji wa nyama umeendelea kuongezeka nchini licha ya bei kuongezeka. Idadi ya mifugo pia imekuwa ikiongezeka.