Wakenya wazua maswali kuhusu mawaziri wateule
Na LUCY KILALO
BAADHI ya watu walioteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta mwezi Januari kuwa mawaziri huenda wakakabiliwa na maswali magumu kutoka kwa Wakenya kuhusu kufaa kwao katika nyadhifa hizo.
“Afisi ya kamati ya Uteuzi imepokea kiapo cha ushahidi wa kuandikwa na barua sita ambazo zinaibua masuala kuhusu uteuzi wa baadhi ya mawaziri,” karani wa Bunge la Kitaifa, Bw Michael Sialai alieleza.
“Pia nimepokea barua nyingine mbili kutoka kwa mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu Kenya (KHRC), Bw George Kegoro na Bw Ekuru Aukot, ambao wangependa kufika mbele ya kamati kuzungumzia masuala ya jumla ya utaratibu wa upigaji msasa.”
Aliongeza: “Umma pia unashauriwa kuwa suala lolote ambalo wangependa kuwasilisha kuhusiana na walioteuliwa, ufanye hivyo wa njia ya kiapo cha ushahidi ulioandikwa.”
Kamati hiyo kisha inatarajiwa kuchunguza barua na ushahidi huo kabla ya shughuli ya kuwapiga msasa mawaziri tisa waliopendekezwa. Rais Kenyatta aliwasilisha majina tisa ya mawaziri wapya kwa Bunge la kitaifa ambao watapigwa msasa na kamati ambayo hatimaye inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake bungeni kuidhinisha ama kupinga mapendekezo yake.
Juma lililopita, kamati hiyo iliondoa tashwishwi yoyote kuhusiana na jinsi itaendesha utaratibu huo, hasa ikibainika kuwa wanakamati ni wa chama tawala cha Jubilee pekee. Upinzani, kupitia kwa Kiongozi wa Wachache, Bw John Mbadi uliandika barua kwa Spika, Justin Muturi na kudumisha msimamo wake kuwa hautashiriki utaratibu huo. Muungano wa NASA umetangaza kuwa hautambui uteuzi huo, kwa kuwa haujatambua serikali iliyopo.
Katika kikao chao cha kwanza juma lililopita, kamati hiyo ilijitetea ikisema kuwa itatekeleza wajibu huo vilivyo. Spika Muturi na Kiongozi wa Walio Wengi katika Bunge la Kitaifa, Adan Duale waliambia wanahabari kuwa wana uwezo wa kuwapiga msasa walioteuliwa, kubainisha utendaji kazi wao.
Wanaotarajiwa kupigwa msasa ni Margaret Kobia (Utumishi wa Umma, Vijana na Mashauri ya Kijinsia), John Munyes (Mafuta na Madini), Monica Juma (Mashauri ya Kigeni), Simon Chelgui (Maji na Usafi), Rashid Echesa (Michezo), Farida Karoney (Ardhi), Ukur Yattany (Leba) Peter Munya (Muungano wa Afrika Mashariki) na Keriako Tobiko (Mazingira).