Wakili amtaka Jumwa kujiuzulu 'kama anajiamini'
NA DANIEL OGETTA
WAKILI Donald Kipkorir anamtaka mbunge wa Malindi Aisha Jumwa kujiuzulu na kuwania ubunge upya kwa chama tofauti na ODM iwapo anaajiamini.
Kupitia kwenye akaunti yake ya Twitter, mwanasheria huyo alimkosoa Jumwa na hata kumshutumu kwa kile alichokitaja kama unafiki.
Kauli hii inafuatia kitendo cha Jumwa kumnyang’anya Bw Edwin Sifuna – ambaye ni katibu mkuu wa ODM – kipaza sauti akipokuwa akihutubia waombolezaji katika hafla ya mazishi Pwani.
Bw Kipkorir alisema kwamba “Aisha Jumwa amekuwa na uraibu wa kukana uhusiano wake na ODM…Ijumaa, alimzuia Edwin Sifuna kuhutubia waombolezaji.”
“Kama anajiamini sana basi ajiuzulu, auwanie ubunge wa Malindi upya kwa tiketi cha chama tofauti na ODM…kwani, Aisha ni mzaliwa wa unafiki na ufisadi,” akasema.
Kauli hiyo ya Bw Kipkorir iliibua hisia kinzani kwani kwenye mtandao huo wa Twitter, watu walionekana kumuunga mkono mwanasheria huyo huku wengine wakimuumbua Bi Jumwa na wengine kumpongeza.
Alipohojiwa kuhusiana na miktadha ya yaliyotendeka katika hafla hiyo ya mazishi, Bw Sifuna alisisitiza msimamo wake kwamba hawezipigana na mwanamke.
“Siiwezipigana na mwanamke. Sijawahi na kamwe sitapigana na mwanamke,” Bw Sifuna alisisitiza.
Bw Sifuna alikuwa amejitambulisha kama mjumbe wa Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga aliyetumwa kuomboleza na familia ya marehemu na kuwasilisha ujumbe wake.
Lakini katika hotuba yake, aligusia umuhimu wa kuheshimu chama cha ODM na kazi yake kama katibu mkuu wa chama kabla ya kukatizwa na Bi Jumwa.
“Mimi naomba nipewe heshima kama mjumbe wa Bw Raila Odinga, heshima ambazo angepokea naomba nipewe ili nipatiane ujumbe. Nina majukumu ya kutimiza na nitayatekeleza bila uwoga na mapendeleo. Sheria ilitungwa na kusema usiwe mkeka wa kulaliwa na kila mtu. Sheria hiyo aliyeitunga sio Sifuna,” alisema.
Alipokuwa bado anahutubia watu, Bi Jumwa alimkatiza akisema, “kwa heshima zote mahali ulipofikia hautaweza kuendelea. Hatuko hapa kusikiliza masuala ya ODM. Tuko hapa kumfariji Kingi. Heshimu Wamijikenda.”
Mbunge huyo ambaye alikuwa amesimama mbele ya jukwaa alielekea moja kwa moja hadi jukwaani na kunyakua kipaza sauti huku akionekana kumchapa Bw Sifuna kichwani na kwenda zake.
“Tafuta jukwa lingine na uzungumze masuala ya ODM. Tuko hapa kufariji wala si kufanya jambo jingine,” aliendelea kusema huku umati ukipiga kelele.
Jana, Wakenya kwenye mitandao ya kijamii waligawanyika kimaoni kwani baadhi walimtetea Bi Jumwa kwa kitendo hicho huku wengine wakimkashifu.
Waliomtetea walisema alifanya jambo la busara kwani haistahili viongozi kupiga siasa mazishini, lakini waliomkosoa walidai huo ni unafiki kwani hata yeye na wenzake walio wandani wa Naibu Rais William Ruto, wamepata umaarufu wa kufanya siasa hadi ndani ya makanisa.
“Je, alifanya hivyo kwa sababu ya jinsi alivyokosana na ODM? Hilo ni kukosa adabu. Viongozi wanafaa waheshimu misimamo inayotofautiana na yao,” akasema aliyekuwa Waziri wa Elimu, Prof James ole Kiyiapi, kwenye mtandao wa Twitter.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria mazishi hiyo ni Gavana wa Kilifi Amason Kingi, Mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya, Michael Kingi (Magarini), Teddy Mwambire (Ganze), Seneta wa Kwale Juma Boi na Mbunge wa Likoni Mishi Mboko.