Wakulima wakashifu wanasiasa kutumia shida za Mumias kujifaa
Na SHABAN MAKOKHA
WAKULIMA wa miwa wametaka wanasiasa wakome kupinga kampuni ya sukari ya Mumias kusimamiwa na mrasimu.
Kulingana nao, wanasiasa sasa wanatumia hali ya Mumias kujitafutia umaarufu wa kisiasa bila kujali maslahi ya wakulima.
“Hatujali ni nani atakayesimamia kiwanda. Kile tunachotaka ni kuona kikifanya kazi. Hatua hii pekee ndiyo itawezesha eneo hili kupata mapato na kutuondolea umaskini,” akasema Bi Atieno Passi, mmoja wa wakulima kutoka Matungu.
Akizungumza wakati wa mazishi ya Paul Netia ambaye ni mwanawe diwani wa zamani Netia Shitawa, mkulima huyo alisema wanasiasa wanajitafutia umaarufu kwa njia isiyofaa.
“Wanatumia jina la kampuni hiyo kujitafutia umaarufu huku mkulima wa miwa akizidi kuwa fukara,” akasema Bw Josphat Waburaka.
Mnamo Septemba 20, Benki ya KCB ilitangaza kuwa Bw PVR Rao atasimamia kiwanda hicho kwani benki hiyo pamoja na mashirika mengine yanadai Mumias Sh12 bilioni.
Ijumaa iliyopita, Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya alialika viongozi wote wa kaunti hiyo kwa mkutano katika ukumbi wa Bishop Stam Pastoral Center kujadiliana kuhusu changamoto zinazokumba Mumias.
Katika mkutano huo, viongozi waliafikiana kuhusu mambo matano kuhusu jinsi ya kufufua Mumias, ikiwemo kwamba wanasiasa watafute nafasi kukutana na Rais Uhuru Kenyatta ili washauriane kuhusu watakavyofufua kampuni hiyo.
“Aidha, tutawasilisha mpango huo kwa wanaodai Mumias ili tuwe na mwelekeo mmoja kuhusu jinsi ya kufufua kampuni hii,” akasema Bw Oparanya.
Viongozi pia walitoa wito kwa asasi za usalama zinazosimamia masuala ya kupambana na ufisadi kukamata watu wanaoshukiwa walipora mali za Mumias.
Aliyekuwa Waziri wa Michezo, Bw Rashid Echesa alisema Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi (EACC), Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) na kitengo cha mashtaka ya umma zinafaa kuchukua hatua mara moja kuchunguza jinsi Mumias ilivyofilisiwa.
Kwa upande wake, Seneta wa Kakamega Cleophas Malala alisema asasi hizo zinahitajika kusaidia Mumias kugharamia madeni yake mengi.
Bw Malala alisema viongozi wa eneo hilo wanashuku huenda KCB ikachukua usimamizi wa kiwanda hicho kisha baadaye kuuza mali zake ikiwemo ardhi, na kufanya ifilisike kabisa.