Wakulima wavuna Sh1.5 bilioni kwenye mnada wa kahawa uliofanyika Jumanne
KIASI cha kahawa kilichouzwa katika Soko la Kahawa la Nairobi (NCE) siku ya Jumanne kiliwaletea wakulima Sh1.5 bilioni.
Jumla ya magunia 28,454 ya kahawa yaliuzwa kwenye mnada huo, yakipungua kwa asilimia 16 kutoka magunia 34,008 yaliyouzwa kwenye mnada wiki iliyopita.
Bei ya wastani kwa kila gunia la kilo 50 ilipungua kidogo hadi Sh44,203.50, ikilinganishwa na Sh45,108 kwenye mnada wa wiki iliyotangulia.
Kiwanda cha Kamoko, chini ya Chama cha Ushirika cha Othaya, kilipata bei bora zaidi baada ya kuuza magunia 51 ya kahawa ya gredi ya AA kwa Sh59,572 kwa kila gunia.
Viwanda vingine vilivyopata bei za kuvutia katika mnada huo ni pamoja na Kathima (Sh55,577), Ndima (Sh54,802), na Gathaithi (Sh54,543) kwa kila gunia la kilo 50.
Katika kundi la mabroka kampuni ya Alliance Berries Ltd iliongoza wengine 12 kwa kuuza magunia 11,603, ambayo yaliingiza Sh602 milioni.
Kirinyaga Slopes iliuza magunia 5,322 ikipata Sh320.5 milioni, Minnesota Coffee Marketers Ltd iliuza magunia 3,254 ikivuna Sh 170 milioni, New KPCU iliuza magunia 2,759 kwa Sh158 milioni, na KCCE iliuza magunia 2,803 kwa Sh161.2 milioni.
Mnada huo uliofanyika katika jumba la Wakulima jijini Nairobi uliwavutia wanunuzi 25, ambapo Ibero Kenya Ltd ilinunua kiasi kikubwa zaidi cha magunia 7,700.
Ibero ilifuatwa na kampuni ya Louis Dreyfus Ltd iliyonunua magunia 4,300, Taylor Winch iliyonunua magunia 3,800, na kampuni ya Sasini ambayo ilinunua magunia 3,400.