Serikali yajinaki imetimiza ahadi tele nusu ya utawala wake
SERIKALI ya Kenya Kwanza imeorodhesha ufanisi wake wa miaka miwili unusu ambayo imekuwa mamlakani, ikitaja hatua kubwa zilizopigwa kwenye sekta za kilimo, afya, elimu, kilimo, nyumba za gharama nafuu miongoni mwa nyingine.
Kwenye ripoti ambayo imeandaliwa na Naibu Mkuu wa Wafanyakazi kwenye Ikulu Eliud Owalo, serikali imesema kuwa imetimiza ahadi zake kwenye sekta hizo ambazo ni msingi wa ukuuaji wa uchumi wa nchi.
Utwala wa Kenya Kwanza umejinaki kuwa katika sekta ya kilimo imepunguza bei ya mbolea kwa asilimia 67. Sasa gunia la mbolea linauzwa kwa Sh2,500 kutoka Sh7,500 mnamo 2022 kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Bw Owalo anayesimamia utekelezaji wa miradi ya serikali.
“Wakulima wamenufaika kutokana na bei ya chini ya pembejeo za kilimo na kupata faida ya juu, wengi wao sasa wakijitosheleza kifedha. Wakulima sasa wanapata mbolea kwa urahisi na kuongeza uzalishaji katika mashamba yao,” ikasema ripoti hiyo.
Katika sekta hiyo hiyo ya kilimo, kiwango cha sukari inayozalishwa kimepanda hadi tani 832, 185 kutoka tani 472, 772. Wakulima wamelipwa deni lote la Sh1.7 bilioni walilokuwa wakilidai huku waajiriwa katika viwanda vya sukari wakipata Sh650 milioni.
Serikali pia inaendelea kujenga nyumba 130,988 mnamo 2025 kutoka 8,872 mnamo 2022. Ujenzi wa nyumba 127, 476 ziaidi unatarajiwa kuanza hivi karibuni kwa kuwa bado hatua ya utolewaji wa zabuni ya ujenzi wao kwa kampuni mbalimbali inaendelea.
Kuhusu ajira, ripoti ya Bw Owalo inasema kuwa nafasi za ajira zilizobuniwa mnamo 2025 imefikia 206,000 kutoka 17,744 hii ikiwa ni ongezeko la nafasi 188,256 ambayo ni asilimia 1,061.
Serikali pia imetenga Sh4.4 bilioni kwenye sekta za Jua Kali na Biashara ndogo ndogo huku pia ikisaidia kuwapiga jeki wafanyabiashara kwenye sekta ya ujenzi.
Bima ya Afya ya Jamii (SHA)ambayo imekuwa ikikabiliwa na matatizo tele nayo imepata ufanisi mkubwa huku Wakenya milioni 19.7 wakiwa wamejisajili mwaka huu.
Mwaka jana watu milioni nane pekee walikuwa wamejisajili SHA Wakenya milioni 4.2 walihamishwa moja kwa moja kutoka Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF).
Hazina Kuu ya Fedha pia ni sehemu ambayo serikali imepiga hatua kubwa kiuchumi ambapo mapato yanayokusanywa nchini yameongezeka kutoka Sh1.9 trilioni mnamo 2022 hadi Sh2.7 trilioni mwaka huu. Hili ni ongezeko la asilimia 42.
Makubaliano ambayo Kenya imekuwa ikitia saini ya kuwatafutia ajira raia wake Uingereza, Mmilki ya Kiarabu, Qatar, Ujerumani na Austria pia yamezaa matunda.
Mnamo 2022 Wakenya 14,651 walipelekwa katika mataifa hayo kupata ajira na mwaka huu idadi hiyo imepanda hadi 202,125. Hata hivyo, Wakenya 2, 741 waliokolewa kutoka kwa mataifa ya nje ambako walikuwa wakiteswa na waajiri wao.
Wakongwe ambao wapo umri wa miaka 70 na zaidi na wanalipwa na serikali kila mwezi pia wameongezeka. Mnamo 2022 walikuwa 732,914 lakini sasa idadi yao ni 1,215, 343 ambayo ni asilimia 66.
Ripoti hii inakuja wakati ambapo Rais William Ruto amekuwa akizuru maeneo mbalimbali kuzindua miradi ya maendeleo na kusema kazi yake ndiyo itasababisha awapiku wapinzani wake mnamo 2027.