Habari

Walimu waingiwa na wasiwasi baada mishahara ya Julai kuchelewa

Na VITALIS KIMUTAI July 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WALIMU wameingiwa na wasiwasi baada ya Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) kuchelewa kutuma mishahara yao ya Julai hata baada ya kutia saini makubaliano mpya kuhusu mishahara (CBA) na vyama vya kutetea maslahi yao.

Zaidi ya walimu 400,000 wanachama wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut), Chama cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo (Kuppet) na Chama cha Kutetea Masilahi ya Walimu wa Shule za Kutoa Elimu Maalum (Kusnet) walipokea nyongeza ya mishahara ya hadi asilimia 29.

Nyongeza hiyo itatekelezwa kwa awamu ndani ya miaka minne.

Imekuwa kawaida kwa TSC kutoa taarifa za malipo ya mishahara kati ya tarehe 24 na 26 kila mwezi ikifuatilia kutuma mishahara siku mbili baadaye.

Lakini hadi tulipoenda mitamboni Julai 28, 2025, TSC haikuwa imetoa taarifa ya mishahara na pesa zenyewe.

Haya yanajiri huku Rais William Ruto akisema Jumapili akiwa Nairobi kwamba serikali yake imetia saini CBA na walimu ili kuzuia migomo ya kila mara na hivyo kuathiri masomo shuleni.

Katibu Mkuu wa Knut Collins Oyuu alisema Jumatatu kwamba walimu wanataka mishahara yao itolewe haraka kuwaondolea wasiwasi.

“Tuko na uhakika kwamba, kulingana na CBA ya 2025-2029 tuliotia saini, nyongeza ya mishahara itatekelezwa kuanzia mshahara wa mwezi huu wa Julai. Chochote kinyume na hiyo hatutakubali,” Bw Oyuu akasema.

Bw Paul Kimetto, Katibu wa Kuppet tawi la Bomet, anasema hofu ya walimu inachangiwa na hali kwamba serikali imekuwa ikilalamikia ukosefu wa fedha za kufadhili miradi mbalimbali nchini. Imekuwa ikidai kuwa kiasi kikubwa cha mapato yake huelekezwa kulipia madeni.

“Ni kweli kwamba kucheleweshwa kwa mishahara kumewatia wasiwasi walimu. Hofu nyingine ni iwapo nyongeza ya mishahara iliyokubaliwa itashirikishwa kwenye mishahara hiyo ya Julai,” Bw Kimetto akasema.

Viongozi wakuu wa TSC walitumia muda wao mwingi katika mazungumzo na viongozi wa vyama vya walimu kabla ya kutiwa saini kwa CBA hiyo mnamo Julai 18, 2025.

Duru zilisema kuwa imewalazimu maafisa wa tume hiyo kufanya kazi kwa saa nyingi hadi wikiendi kuhakikisha kuwa nyongeza hiyo inashirikishwa katika mishahara ya Julai.

Duru katika TSC zilisema Jumatatu kuwa kazi hiyo imekuwa ngumu na imewavuta maafisa hao kwa majuma mawili sasa.

“Kuandaa jedwali mpya inayoakisi nyongeza ya mishahara ya walimu wa gredi tofauti, kuthibitisha maelezo yao na kuyaweka kwenye mitandao wa TSC ni kazi ngumu inayochukua muda na nguvu. Kosa ndogo itagharimu tume pesa nyingi zaidi,” afisa mmoja, ambaye haruhusiwi kuongea na wanahabari, aliambia Taifa Leo.

Endapo TSC na vyama vya walimu zingefeli kuelewana mishahara ya walimu ingetayarishwa haraka.

Mwenyekiti wa TSC Jamleck Muturi na Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji Evaleen Mitei waliwakilisha tume hiyo kwenye meza ya mazungumzo na vyama vya walimu kuhusu CBA hiyo mpya.

Mkataba huo ulitiwa saini saa za usiku Ijumaa Julai 18 katika Taasisi ya Elimu Maalum Nchini (KISE) eneo la Kasarani, Nairobi.