Waliofumaniwa harusini watengwa kwa lazima kwa gharama yao
Na MARY WANGARi
Kioja kilizuka Jumaatatu baada ya maafisa wa polisi kuwafumania wanawake 39 harusini licha ya marufuku ya serikali dhidi ya mikusanyiko ya umma kuhusiana na kuenea kwa Covid-19.
Wanawake hao walikuwa wamehudhuria harusi ya mwenzao katika eneo la Nasra, Komarock, jijini Nairobi kabla ya kupatikana na polisi waliokuwa wakipiga doria.
Kulingana na Kamanda wa Polisi katika Eneo la Kayole, Wilson Kosgey, wanawake hao sasa watatengwa kwa lazima katika kituo cha karantini cha KMTC ambapo watahitajika kugharamia wenyewe siku 14 watakazokaa humo.
Kupitia video ilyosambazwa mno mitandaoni, wanawake hao wanaonekana waking’ang’ana kufunika nyuso zao kwa kutumia chochote walichotia mikononi mwao ikiwemo vitambaa na buibui zao, baada ya kufumaniwa na polisi wakiwa bila barakoa.
Afisa mmoja wa polisi anasikika akiwauliza wanawake hao kwa lafudhi ya Kisomali ni kwa nini hawakuwa wakizingatia kanuni kuhusu Afya ya Umma inayohitaji watu kuvaa barakoa wanapotangamana.
“Serikali inasema mfungue mapua. Mbona hamjafanya hivyo?” anauliza afisa huyo huku wanawake hao wakifurukuta kujifunika nyuso zao.
Hata hivyo, juhudi zao ziliambulia patupu huku baadhi yao wakiamua kuungama na kuomba msamaha baada ya kugundua adhabu iliyowasubiri kwa kukiuka marufuku ya serikali dhidi ya mikutano ya watu zaidi ya 15.
“Tunakubali makosa yetu, tuko na makosa. Lakini nyinyi mjue makosa yenu. Mnajua hakuna harusi inakubaliwa inakubaliwa watu wachache. Hiki kitendo kimefanyika kwa sababu ya Mwenyezi Mungu,”
Kulingana na mmoja wao, harusi hiyo ilipangiwa watu wachache lakini wengine ambao hawakuwa wamealikwa wakahudhuria.
“Hii harusi tulikuja watu wachache. Kisha wasichana wachache ambao sisi hatukuwaalika wakaja. Tunataka kufuata sheria, tuko na haki kama wamama. Hata kama tumeshikwa tungepelekwa kituo cha polisi,” alilia mama mmoja ambaye hakujitambulisha.
Kisanga kilizuka wakati mama mmoja mwenye umri wa makamo alipopanda kwenye dari katika juhudi za kukwepa kukamatwa na maafisa hao.
Maafisa wa polisi walipigwa na butwaa walipomwona mwanamke huyo akishuka kutoka juu ya jumba hilo linaloendelea kujengwa, wakisalia kushangaa jinsi alivyoweza kupanda licha ya umri wake.
Kisa hiki ni mojawapo wa misururu ya matukio ambapo Wakenya wanaibuka na visanga vya kila namna katika juhudi za kukwepa marufuku ya kuingia na kutoka kaunti husika, saa za kafyu pamoja na masharti kuhusu kuvalia barakoa katika juhudi za kudhibiti maambukizi ya Covid-19.
Hivi majuzi tu, Wakenya waliachwa vinywa wazi wakati kundi la watu lilikodisha gari na kununua jeneza ili kuweza kusafiri kutoka kaunti ya Nairobi hadi kaunti ya Homabay ambapo walinaswwa na maafisa wa polisi.
Watu hao walipelekwa katika kituo cha karantini ambapo dereva wa gari hilo alipatikana kuwa na virusi vya corona.
Haya yote yanajiri huku kukiwa na wasiwasi kwamba idadi kubwa ya Wakenya hawatilii maanani mikakati iliyowekwa ba Wizara ya Afya ya kusaidia kuzuia kusambaa kwa gonjwa hilo ambalo kufikia sasa jumla ya watu 281 wameambikizwa.