Waliomwapisha Raila wajuta
Na VALENTINE OBARA
WANDANI wa Kiongozi wa Chama cha ODM Bw Raila Odinga, ambao walikuwa katika mstari wa mbele kumwapisha kuwa ‘rais wa wananchi’ baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2017, sasa wanajuta kwa hatua yao.
Bw Odinga alikula kiapo hicho Januari 2018 kukiwa na taharuki kuu nchini baada ya muungano wake wa NASA kususia uchaguzi wa marudio, na kupelekea Rais Uhuru Kenyatta kuibuka mshindi.
Walioonekana kumshinikiza zaidi kula kiapo walikuwa ni Mwanauchumi David Ndii, aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnstone Muthama na mwanaharakati Miguna Miguna.
Kwenye mahojiano tofauti, watatu hao wameonekana kuwa na msimamo mmoja kwamba kiapo cha Bw Odinga kilistahili kupigania masilahi ya raia na kuleta mabadiliko ambayo yatarekebisha hali ya maisha kwa mwananchi wa kawaida.
Tofauti na lengo hilo, maoni yao ni kuwa Bw Odinga alisaliti malengo hayo kwa kujiunga na Rais Kenyatta kupitia kwa handsheki ya Machi 2018, na matokeo yake ikawa ni kupigania marekebisho ya katiba ya kibinafsi kati yao wawili.
Kulingana na Bw Muthama, marekebisho ya katiba pekee jinsi inavyoshinikizwa hayatatatua changamoto zinazokabili nchi hivi sasa.
Kulingana naye, kile kilichohitajika zaidi ni kubadilisha viongozi wa nchi ili kuwe na viongozi wenye maono yanayoweza kukabiliana kikamilifu na ufisadi na gharama ya juu ya maisha.
“Tukibadilisha katiba na viongozi wale wale ndio watabaki mamlakani, hatutakuwa tumebadilisha chochote isipokuwa mbinu za wizi,” akasema alipozungumza Jumapili katika Kanisa la AIC Muthetheni, Kaunti Ndogo ya Mwala.
Bw Odinga amekuwa akishinikiza kuwe na marekebisho ya katiba yatakayobadili mfumo wa uongozi ili kuwe na nafasi ya waziri mkuu mwenye mamlaka makubwa na manaibu wake.
Msimamo sawa na wa Bw Muthama ulitolewa na Dkt Ndii, ambaye alifafanua kwamba haungi mkono BBI licha ya kuwa mwandani mkubwa wa Bw Odinga wakati wa uchaguzi wa 2017.
“Ninapinga vikali utumizi wa katiba kuendeleza masilahi ya watu binafsi ya kisiasa. Tatizo kuu lililopo ni kuhusu ukwepaji wa sheria kwa kutumia vibaya mamlaka, ukiukaji wa katiba kupita kiasi ikiwemo ukiukaji wa maadili, ukandamizaji wa demokrasia kupitia utapeli uchaguzini miongoni mwa mengine,” akasema.
Kwa upande wake, Dkt Miguna ambaye ndiye aliyeathirika zaidi kwa kumwapisha Bw Odinga, ameshikilia kuwa walipomwapisha walikuwa na matumaini kuwa angetetea haki za wananchi, lakini kwa mtazamo wake handisheki ilikuwa ni jambo la ubinafsi kati ya kigogo huyo wa kisiasa na Rais Kenyatta.
Dkt Miguna, ambaye alifurushwa akapelekwa Canada, amedai BBI ambayo iliyokana na handisheki ni njama ya kuwezesha familia za wawili hao kukaa mamlakani kwa muda zaidi.