Wanafunzi 261,000 hawajulikani walipo mitihani ya kitaifa ikianza rasmi
ZAIDI ya wanafunzi 261,000 waliotarajiwa kuendelea na masomo na kufanya mitihani ya kitaifa mwaka huu hawajulikani walipo, hali inayozua maswali kuhusu sera ya serikali ya kuhakikisha wanafunzi wote kutoka shule ya msingi wanajiunga na zile za sekondari.
Takwimu za Baraza la Kitaifa la Mitihani Kenya (KNEC) zinaonyesha kuwa watahiniwa 1,233,852 walifanya mtihani wa KCPE mnamo 2022.
Hata hivyo, ni wanafunzi 1,048,355 pekee waliojisajili kufanya mtihani wa KCSE mwaka huu, pengo la wanafunzi 185,497.
Vilevile, wanafunzi 1,281,210 walifanya tathmini ya KPSEA mnamo 2023, lakini waliojisajili kufanya tathmini ya KJSEA mwaka huu ni 1,206,028. Hii ni tofauti ya wanafunzi 75,182.
Kwa jumla, wanafunzi 260,679 hawapo katika makundi yaliyotarajiwa kuendelea hadi mitihani inayofuata.
Hata hivyo, tofauti hiyo haimaanishi kwamba wote waliacha shule, kwani huenda baadhi walifariki, wakahamia mifumo mingine ya elimu au kuchelewa kuendelea na masomo. Waziri wa Elimu Julius Ogamba alisema sababu kadhaa zinaweza kueleza tofauti hiyo.
“Baadhi ya upungufu huu unatokana na hali za kawaida, ikiwemo wanafunzi waliofariki au ambao hawawezi kuendelea na masomo. Wengine wamehamia mifumo mbadala ya elimu kama shule za kimataifa,” akasema.
Aliongeza kuwa baadhi ya wanafunzi huacha shule kwa muda kutokana na mimba za mapema au maradhi, lakini huruhusiwa kurejea na kuendelea na masomo.
Wakati huo huo, wanafunzi wa Gredi ya Sita na Gredi ya Tisa wanaanza tathmini za kitaifa, huku mitihani ya KCSE ikiendelea kote nchini. Jumla ya watahiniwa 3,634,846 wamejisajili kwa mitihani na tathmini hizo tatu.
KNEC imetuma maelfu ya wasimamizi kuhakikisha zoezi hilo linaendeshwa kwa usalama. Mkurugenzi mkuu wa baraza hilo, David Njengere, alisema simu hazitaruhusiwa wakati wa mitihani ya KCSE.
“Kukiuka sheria hii kutachukuliwa kuwa udanganyifu wa mtihani kwa mujibu wa sheria na kanuni za KNEC,” akasema.
Baraza hilo pia zinatumia kufuli zenye nembo ya usalama kwenye kontena za kuhifadhi karatasi za mitihani ili kuimarisha usalama.
Hata hivyo, mgogoro kuhusu malipo ya walimu wanaosimamia mitihani bado unaendelea.
Muungano wa Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Anuwai (KUPPET) ummewataka wanachama wake kujiepusha na shughuli za KNEC hadi malalamishi yao yatakapotatuliwa.
Naibu katibu mkuu wa chama hicho, Moses Nthurima, alisema suala si kulipwa kwa wakati pekee, bali pia kiwango cha malipo.
“Tunasisitiza kuwa walimu hawapaswi kujihusisha na shughuli za mitihani kwa sababu hiyo ni aina ya utumwa,” akasema.
Wakati huo huo, wakuu wa shule wameiomba Bunge kusitisha ukaguzi na ziara za maafisa wa serikali shuleni hadi mitihani imalizike, wakisema shughuli hizo zinawavurugia maandalizi.
Hata hivyo, Spika Moses Wetang’ula alisema uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma hauwezi kusitishwa.
“Uwajibikaji kuhusu matumizi ya rasilimali za umma si jambo la hiari. Ni wajibu wa kikatiba,” akasema.