Jengo la mauti Eastleigh : Sakaja awalaumu polisi
GAVANA wa Nairobi Johnson Sakaja amelaumu polisi kwa kuwaachilia washukiwa waliohusishwa na ujenzi wa jengo lililoporomoka Eastleigh.
Bw Sakaja amewataka maafisa wa usalama waeleze kwa nini watu waliokamatwa kwa kukiuka sheria za mipango ya miji waliachiliwa kwa dhamana ya Sh50,000 bila kufikishwa mahakamani.
Gavana huyo alisema maafisa wa kaunti walikagua eneo hilo na kubaini kuwa ruhusa ya kubadilisha matumizi ya ardhi ilikuwa imetolewa, lakini mipango ya usanifu iliyohitajika kuidhinisha ujenzi haikuwa imeidhinishwa.
Alisema kaunti iliwakamata washukiwa na kuwakabidhi katika Kituo cha Polisi cha Kamukunji, lakini baadaye baadhi yao wakaachiliwa.
“Tulitekeleza sheria na kuwakamata waliohusika na kwa kuwa hatuna mamlaka ya kuendesha mashtaka, washukiwa walikabidhiwa polisi. Inaripotiwa kuwa waliachiliwa kwa dhamana ya Sh50,000 bila kufikishwa mahakamani,” akasema. Rekodi za polisi zinaonyesha washukiwa 14 waliwekwa kizuizini Juni 17, 2026, kwa makosa yanayohusiana na ukiukaji wa sheria za mipango miji.
Hata hivyo, rekodi nyingine zinaonyesha washukiwa 10 waliachiliwa kwa dhamana kwa maagizo ya mkuu wa kituo hicho, hali inayozua maswali kuhusu kilichowapata wengine.
Wakati viongozi wakilaumiana, familia za watu waliopotea katika mkasa huo zinaendelea kusubiri habari za wapendwa wao.
Kufikia Jumapili adhuhuri, familia 47 zilikuwa zimeripoti ndugu zao kutoweka, ingawa tisa zilikuwa zimeunganishwa tena na jamaa zao, kulingana na Katibu wa Wizara Susan Mang’eni.
Dina Mueni amekuwa katika eneo la mkasa tangu Ijumaa akimtafuta dada yake, Eunice Mwikali, 41, aliyekuwa akifanya kazi ya ushonaji katika jengo hilo.
“Kama anaweza kupatikana, nitashukuru sana. Si rahisi kumtafuta mtu bila kujua kama yu hai au amefariki,” akasema Bi Dina.
Hata hivyo, manusura Victor Onyango amewapa familia hizo matumaini. Fundi huyo wa ushonaji alinaswa chini ya vifusi Ijumaa, lakini akaokolewa Jumamosi akiwa na majeraha madogo.
“Ninamshukuru Mungu sana,” alisema. Hata hivyo, mashine zake tatu za kushona na biashara yake zilibaki chini ya vifusi.