Habari

Wanafunzi wapya kabisa chekechea kuingia shuleni Julai 2021

November 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na FAITH NYAMAI

WANAFUNZI wapya kabisa chekechea PP1 wataingia shuleni Julai 2021, imesema Wizara ya Elimu wakati waziri George Magoha akisema shule zote zitafunguliwa upya Januari 4, 2021, tangu zilipofungwa Machi 2020 kwa sababu ya janga la Covid-19.

Kalenda ya shule inaonyesha kwamba sasa muhula wa pili utakamilika Machi 19, 2020.

Wanafunzi wataenda nyumbani kwa likizo ya wiki saba katika kipindi ambacho mchakato wa kusahihisha mitihani ya kitaifa utakuwa umeanza.

Prof  Magoha amesema wanafunzi wa PP1 na PP2, wale wa Darasa la Kwanza hadi Darasa la Tatu, wale wa Darasa la Tano hadi la Saba halafu wale wa Kidato cha Kwanza hadi Kidato cha Tatu, watakuwa wanaanza muhula wa pili hiyo Januari.

Tayari Wanafunzi wa Gredi ya Nne, Darasa la Nane na Kidato cha Nne wako shuleni kumaanisha watakuwa wanaingia shuleni kwa muhula wao wa tatu hiyo Januari.

“Shule zote zitafunguliwa upya Januari 4, 2021, na hii ni kwa wanafunzi wa sasa wa PP1 na PP2, Gredi ya Kwanza hadi Gredi ya Tatu, Darasa la Tano hadi Darasa la Saba na Kidato cha Kwanza hadi Kidato cha Tatu,” amesema Prof Magoha baada ya kukutana na wadau wa sekta ya elimu katika Taasisi ya Kukuza Mitaala Nchini (KICD), Nairobi.

Sasa wanafunzi wapya kabisa wanatarajiwa kuingia shuleni Julai mwakani.

Mitihani ya KCPE na KCSE imeratibiwa kuanza Machi 2021.