SERIKALI imepanga kuitisha mkutano wa ngazi ya juu wiki ijayo ili kukamilisha mpango wa kuwawezesha wanafunzi wa Chuo cha Mafunzo ya Utabibu Kenya (KMTC) kupata ufadhili kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (Helb).

Hatua hiyo inayotajwa kuwa mageuzi makubwa katika ufadhili wa masomo ya taaluma ya afya.

Profesa Kindiki alisema serikali imeidhinisha ombi la KMTC la kuwajumuisha wanafunzi wake katika mpango wa Helb, na kwamba atakutana na maafisa kutoka Wizara ya Afya, Elimu na Wizara ya Fedha ili kukubaliana kuhusu mfumo wa utekelezaji.

Alizungumza hayo Alhamisi wakati wa mahafali ya 94 ya KMTC, ambapo pia alionya kuwa Kenya inaendelea kukabiliwa na uhaba mkubwa wa wahudumu wa afya licha ya kutoa maelfu ya wahitimu kila mwaka.

Kwa sasa, Kenya ina jumla ya wahudumu wa afya 230,000 ilhali inahitaji 310,000, ikiwa na upungufu wa takriban 80,000.

Prof Kindiki alisisitiza kuwa afya ya wananchi ni nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa, akiongeza kuwa serikali inapanua fursa za ajira kwa wataalamu wa afya ndani na nje ya nchi.

Alisema serikali imezindua mpango wa kutengeneza nafasi za ajira nje ya nchi kwa wahudumu wa afya, ikiwemo Canada.

Kuhusu mzigo wa matibabu kwa familia, Naibu Rais alisema kuwa karibu Wakenya milioni 28 sasa wanahudumiwa chini ya mfumo mpya wa bima ya afya ya kijamii, ikilinganishwa na milioni 7.5 mwaka 2022.

Alieleza kuwa kuanzishwa kwa Mamlaka ya Bima ya Afya ya Jamii (SHA) kutaongeza zaidi upatikanaji wa huduma bora za afya.

“Ushirikiano wa kupiga jeki vifaa vya kitabibu na kuimarisha mifumo ya usambazaji dawa unaendelea ili kuhakikisha dawa na vifaa vingine vinafika hospitalini kwa wakati na kwa viwango vinavyohitajika,” alisema.