Wanaharakati wataka Magoha atimuliwe kazini
Na DENNIS LUBANGA
MASHIRIKA ya kutetea haki za kibinadamu kutoka eneo la Bonde la Ufa, sasa yanamtaka Rais Uhuru Kenyatta kumfuta kazi Waziri wa Elimu Profesa George Magoha kufuatia dai alimtusi Mkurugenzi wa Elimu Kaunti ya Uasin Gishu Dkt Gitonga Mbaka.
Wanaharakati hao wanasema tabia ya waziri huyo ilionyesha kuwa hafai kushikilia afisi ya umma.
Wakiongozwa na Bw Kimutai Kirui kutoka Kituo cha Against Torture mjini Eldoret, wameshutumu EACC kwa kumdhulumu Dkt Mbaka na maafisa wengine wa umma.
“Tunahofia kwamba Dkt Mbaka anadhulumiwa kwa njia moja au nyingine kwa sababu hatujaona Bw Magoha akiitwa kuandikisha taarifa yake. Profesa Magoha ndiye mwenye kosa na Dkt Mbaka ndiye mhasiriwa. Tunaona mhasiriwa akiitwa bila kujua anakokwenda au kesi hiyo imefika wapi,” alisema
Walidai kwamba badala ya Profesa Magoha kuchukuliwa hatua kwa kumdunisha, ni Dkt Mbaka na maafisa wengine wa elimu na utawala ambao wanatakiwa kuandikisha taarifa.
Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) ilimuita Dkt Mbaka kuandikisha taaarifa na imewaita maafisa wengine pia.
Miongoni mwa waliohojiwa na EACC ni Mkurugenzi wa Elimu Kaunti ndogo ua Kapseret (SCDE), Naibu Kamishna Kapseret na Naibu Kamishna katika Kaunti.
Wengine ni pamoja na mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Langas waliofika mbele ya Tume hiyo mnamo Jumanne naye Naibu Mwalimu Mkuu alipangiwa kuhojiwa jana.
Mkurugenzi wa Elimu Kesses na Waziri Magoha wamepangiwa kujiwasilisha mbele ya Tume hiyo katika tarehe itakayotajwa baadaye.
“Hatutaki wanyanyasaji katika afisi zetu. Kitendo hicho ni ukiukaji wa wazi wa sheria na matumizi mabaya ya afisi. Magoha anapaswa kwenda nyumbani. Ninahofia kwamba Dkt Gitonga ambaye ndiye mhasiriwa huenda akakosa kupata haki kwa sababu aliyemdhulumu hajaitwa kujiwasilisha kuandikisha taarifa,”
Bw Kirui alisema kwamba suala hilo linahusu maadili na EACC ilipaswa kulifuatilia tangu mwanzo na kwenda katika afisi ya Bw Mbaka kuandikisha taarifa badala ya kumuita hata kabla ya kuandikisha taarifa kutoka kwa waziri huyo.
Mnamo Jumatano, Bw Mbaka alikataa kuzungumza na vyombo vya habari baada ya kuhojiwa kwa muda wa saa tatu na EACC. Aliondoka kwa kasi akitumia gari lake rasmi punde tu baada ya kutoka afisi hiyo.
Dkt Mbaka anatarajiwa kustaafu Machi mwaka ujao baada ya kuhudumu kwa zaidi ya miaka 35.
Waziri alimfedhehesha Dkt Mbaka alipoenda katika Shule ya Msingi ya Langas kukagua Mradi wa kupeleka madawati kabla ya masomo kurejelewa mnamo Januari.
Afisa huyo wa elimu alirekodiwa kwenye video akimzomea Mkurugenzi huyo wa kaunti kwa njia ya kumdhalilisha na hata kumwita mjinga.
Bw Kirui alisema kwamba kinachohitajika kuhakikisha maadili yamedumishwa ni kuchukulia hatua maafisa wa serikali wanaoyakiuka.
Kufuatia tukio hilo, Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) ilimvua waziri Magoha jukumu la kusimamia wafanyakazi wa wizara yake lakini akapuuza akisema ni rais pekee anayeweza kumwelekeza jinsi ya kufanya kazi yake.