HabariSiasa

Wanaotaka kuning'oa mamlakani wanaota mchana – Ruto

March 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

WAANDISHI WETU

NAIBU RAIS William Ruto, amewapuuzilia mbali wale wanaoendeleza mpango wa kumuondoa mamlakani akisema ataendelea kushikilia wadhifa wake hadi 2022.

Akiongea kwa mara ya kwanza tangu seneta wa Siaya James Orengo atangaze kuwa atawasilisha bungeni hoja ya kumng’oa mamlakani, Dkt Ruto alisema hakuna hoja kama hiyo inayoweza kumtisha.

“Wanakerwa kwamba Ruto yuko hapa na pale. Je, tuko na manaibu rais wawili nchini Kenya. Niko hapa, sasa shida iko wapi?” aliuliza alipoongoza shughuli ya kuchanga fedha za kusaidia kundi la akina mama katika uwanja wa michezo wa Hamisi, Kaunti ya Vihiga.

Alisema hayo huku Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kikisema hoja ya kumtoa uongozini kwa tuhuma za ufisadi ni ya dharura.

Katibu wa chama hicho Bw Edwin Sifuna alisema akiwa kaunti ya Kilifi kwamba, chama hicho kinafikiria njia kadhaa ambazo zitamuondoa Naibu Rais uongozini.

Bw Sifuna alisema kuwa chama cha ODM kitaendelea kuzungumza ukweli kuhusu ufisadi ambao umekithiri nchini bila kuogopa.

“Hatutaogopa mtu yeyote katika vita hivi dhidi ya ufisadi. Lazima kieleweke. Tutafichua ufisadi mchana na usiku na hata kama watatuua, tutakuwa tumesimama na hatutaogopa,” akasema Bw Sifuna.

Hata hivyo Bw Ruto alitaja mjadala huo kama mbinu za kulemaza ajenda ya serikali ya Jubilee.

Akionekana kumrejelea kiongozi wa ODM Raila Odinga, Dkt Ruto aliwaonya wapinzani wake dhidi ya kupanga njama ambazo zinalenga kuwanufaisha wao wenyewe akiwataka kuendeleza siasa zenye manufaa kwa Wakenya wote.

“Tunataka kuwaambia marafiki zetu kwamba tunataka kufanyakazi katika masuala ya maendeleo. Wasituletee mambo yasiyo na manufaa na yenye kuleta migawanyiko miongoni mwa Wakenya. Tunataka kuunganisha wananchi, tunataka kutekeleza Ajenda Nne Kuu za Maendeleo,” alisema.

Akiongea katika eneo bunge la Ugenya wikendi iliyopita, Bw Orengo alisema atawasilisha hoja ya kumuondoa mamlakani Dkt Ruto kwa kuhujumu vita dhidi ya ufisadi vinavyoendelezwa na serikali.

“Ikiwa Ruto amekataa kujiuzul, nitamuondoa kupitia kura ya hoja bungeni kwa kuzingatia kipengee cha 150 (1) (b) kinachotoa mwanya kwa naibu rais kuondolewa mamlakini kutumia mchakato wa kisiasa,” akasema Bw Orengo alipohutubia mkutano wa kampeni katika kijiji cha Sifuyo.

Kauli ya Seneta huyo wa Siaya ilichochea mjadala mkali wa kisiasa huku wandani wa Dkt Ruto wakidai nia yake ni kumwezesha Bw Odinga kuchukua wadhifa huo na hivyo kuzima ndoto ya naibu rais kuingia Ikulu 2022.

“Tunajua Orengo ni mtu wa mkono wa Odinga. Yeye, Raila, ndiye anataka Naibu Rais William Ruto aondolewe ili achukue kiti hicho kwa njia ya mkato.. lakini tunataka kumwambia kwamba Jubilee iko imara na mipango hiyo kamwe haitafaulu,” akasema mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro aliyewaongoza wenzake 15 kukashifu Bw Orengo.

“Tunataka kumwambia Raila kwamba njia ya kipekee ya kupata mamlaka ni kwa Raila na wenzake katika ODM kujiwasilisha kwa wananchi ili apigiwe kura. Sio kutumia Orengo kuwasilisha hoja ambayo haina mantiki yoyote kikatiba,” aliongeza.